Bayern mabingwa wa Bundesliga kwa mara ya tano mfululizo
1 Mei 2017Kikosi hicho cha kocha Carlo Ancelotti kimepanua mwanya kwa ushindi huo dhidi ya timu ya pili katika msimamo wa ligi RB Leipzig hadi pinti 10 na kwa hiyo katika michezo mitatu iliyosalia katika msimu huu wa ligi haitawezekana tena kuzifikia pointi hizo na kuwapiku mabingwa hao.
Huyu hapa mwenyekiti wa Bayern Munich Karl-Heinz Rummenigge. "Kwa bahati mbaya , katika Champions dhidi ya Real Madrid kulikuwa na uamuzi fulani wa refa haukuwa mzuri. Na katika kombe la Ujerumani pia dhidi ya Dortmund bahati haikuwa upande wetu. Pia tunacheza katika wiki za mwisho vizuri , lakini kwa bahati mbaya pamoja na hayo tumetolewa. Ni ubingwa wa Bundesliga tu ndio unawezekana, ambapo katika mchezo wa 34 haitakuwa furaha , ama bahati mbaya. Kwamba unastahili ushindi ama la. Na nafikiri , timu yetu imethibitisha , kwamba wanastahili kuitwa mabingwa halisi wa Ujerumani msimu huu kwa mara nyingine tena.
"Si rahisi , kwamba katika Bundesliga unaweza kushinda tu, " amesema nahodha wa Bayern akiwa na furaha tele Philipp Lahm baada ya ushindi wa jumla ya mataji manane ya ubingwa wa Ujerumani. Nahodha huyo anatundika madaluga baada ya msimu huu.
RB Leipzig iliyotarajiwa kuahirisha sherehe za ubingwa wa Bayern , iwapo ingeishinda timu iliyoko mkiani mwa ligi Ingostadt,ilishindwa kufanya hivyo na iliridhika na sare ya bila kufungana na kuipa matumaini Ingolstadt angalau kwa muda tu kuweza kubakia katika daraja la kwanza. Kwa sare hiyo Ingolstadt imeongeza katika matumaini yake kwa kuwa na pointi 29 pointi nne tu kutoka nafasi ya 16 ambayo inatoa matumaini ya kucheza na timu ya tatu ya daraja la pili kuamua nani anaingia ama kubaki katika daraja la kwanza. Nahodha wa Ingoltadt Marvin Matip ameonesha matumaini.
"Ndio , nafikiri mtu akiangalia kwamba katika dakika kumi za mwisho tulicheza tukiwa pungufu , hii ni pointi moja tuliyoipata kutokana na ari. Tuna bado michezo miwili nyumbani , na mchezo mmoja ugenini dhidi ya Freiburg. Nadhani bado tuko hai. Nimefarijika , kwamba tunaishi na dhidi ya timu ngumu kama Leipzig kupata pointi moja , ni sawa kabisa."
Timu iliyoko katika nafasi ya mwisho kabisa katika Bundesliga msimu huu SV Darmstadt 98 ilijitutumua nayo katika mchezo huu wa 31 na kuikaba koo FC Freiburg na kuishinda bila kutarajiwa kwa mabao 3-0, na kufufua pia matumaini yao ya kubakia katika daraja la kwanza.
Hata hivyo karibu nusu ya timu za Bundesliga zinajikuta baina ya kuwania nafasi ya kucheza katika ligi ya Ulaya na hofu ya kushuka daraja. Hamburg SV imejikuta tena wiki hii ikirejea katika madhila yaliyowakuta misimu miwili iliyopita ya kukaribia kusuka daraja. Msimu huu pia hali imeanza kujitokeza kuwa hivyo. Hamburg iliangushiwa kipigo cha mabo 4-0 dhidi ya Augsburg katika mchezo ambao timu zote zilikuwa katika eneo la hatari ya kushuka daraja. Kwa ushindi huo Augsburg imechupa kutoka nafasi ya 16 hadi nafasi ya 13 ,ikiwa na pointi 35 , ikizivuta chini Mainz 05, Wolfsburg na Hamburg SV ambazo zote zina pointi 33.
Michezo mitatu iliyobaki katika Bundesliga itaamua nani anashuka daraja miongoni mwa timu hizo. Lakini pia wasi wasi umetanda miongoni mwa timu saba za Bundesliga, ambazo kila moja inaweza kuliaga daraja hilo. Timu hizo ni Schalke 04 , Eintracht Frankfurt, Bayer 04 Leverkusen , Augsburg, Mainz 05 , Wolfsburg na Hamburg ambazo zinaweza kushuka daraja.
wakati huo huo timu za Borussia Moenchengladbach, FC Koloni, Freiburg, Werder Bremen na Hertha Berlin zote zina nafasi kuingia katika kinyang'anyiro cha ligi ya Ulaya mwakani zikiwa na pointi zinazotofauti kwa kiasi kidogo tu kabla ya michezo hii mitatu ya mwisho kufikia mwisho.
Mfutano hata hivyo uko baina ya makamu bingwa msimu uliopita Borussia Dortmund na 1899 Hoffenheim. Wazee wa kijijini Hoffenheim wakiwa katika msimu wao bora kabisa tangu timu hiyo kuingia katika Bundesliga , wameipiku Borussia Dortmund jana katika nafasi ya 3 ambayo inawahakikishia kucheza katika awamu ya makundi ya Champions League msimu ujao moja kwa moja. Hoffenheim iliikandika Eintracht Frankfurt jana Jumapili kwa bao 1-0 na kufikisha pointi 58 dhidi ya 56 za Borussia Dortmund ambayo iliambulia sare ya bila kufungana na FC Kolon siku ya Jumamosi.
Kocha wa Frankfurt Nico Kovac alichooka sana: "Inauma sana , wakati unashindwa katika dakika za mwisho kutokana na mpira wa adhabu , wakati kila kitu kimsingi kilikuwa katika hali nzuri kabisa . Kikosi changu kilitoa kila kitu , ambacho mwili unacho. Bahati mbaya haikuwezekana kufaidika na hilo, kwasababu tulifumba jicho kwa sekunde tu."
Katika mchezo wa 32 wa Bundesliga , vumbi litatimka katika uwanja wa Signal Iduna Park mjini Dortmund wakati Borussia Dortmund itakapowakaribisha wazee wa kijijini Hoffenheim katika kinyang'anyiro cha kuwania nafasi ya tatu na pia Koln ikiikaribisha Werder Bremen katika kuwania nafasi ya kucheza Ulaya. lakini pia Hamburg iliyoko katika nafasi ya 16 inatafuta kujinasua kutoka katika hatari ya kushuka daraja wakati itakapoikaribisha nyumbani Mainz 05 ambayo nayo ina pointi sawa na Hamburg zitakapooneshana kazi kuepuka kushuka daraja.
Mwandishi: Sekione Kitojo / rtre / afpe / dpae
Mhariri: Iddi Ssessanga