Bayern Munich kidedea, Marco Reus arejea uwanjani
12 Februari 2018Bayern Munich imeendelea kuonesha ubabe wake katika ligi ya Ujerumani Bundesliga, ambapo Jumamosi hii iliizaba Schalke 04 kwa mabao 2-1 ikiwa nyumbani, wakati ambapo kocha wake mkuu Jupp Heynckey hakuwapo uwanjani kuiongoza timu hiyo kutokana na kuugua homa.
Bayern inaongoza kwa pointi 18 , ikifuatiwa na RB Leipzig ambayo wiki iliyopita ilikuwa katika nafasi ya tatu, na nafasi hiyo ya pili ikishikiliwa na Bayer Leverkusen.
Lakini baada ya Bayer Leverkusen kushinda katikati ya wiki katika mchezo wa kombe la shirikisho nchini Ujerumani DFB Pokal dhidi ya Werder Bremen, kwa mabao 4-2, ushindi huo uliigharimu timu hiyo kwa kuwa wachezaji walionekana kuwa na miguu mizito na kukubali kipigo cha mabao 2-0 nyumbani dhidi ya Hertha BSC Berlin. Akielezea kuhusu mbinu za mchezo huo zilivyopangwa na kocha mkuu wa Hertha Berlin Pal Dardai , mchezaji wa kati wa Hertha Valentino Lazaro aliyefunga bao muhimu la pili katika mchezo huo alisema.
"Kazi yangu leo ilikuwa kukaa kwa muda mfupi sana na mpira, badala yake kucheza kwa pamoja zaidi na kufanya haraka kuelekea katika lango la adui. Kulia sikuwa napata mipira ya mara nyingi, kwa hiyo nikabadilisha upande, kwa kuwa nilikuwa na hisia kwamba adui ametambua mbinu hiyo. bila shaka baada ya kushika mpira wa kwanza ama wa pili kila kitu kilikuwa sahihi. Nimefurahi sana jinsi mambo yalivyokwenda na nafarijika kuhusu pointi tatu leo."
Kwa mara ya kwanza katika mwaka huu wa 2018 , Borussia Dortmund imeweza kupata pointi zote tatu katika uwanja wake wa nyumbani , baada ya kutoka sare mara mbili.
Marco Reus arejea uwanjani
Lakini habari hizo nzuri kwa mashabiki wa Borussia Dortmund ziliongezewa hamasa baada ya kuonekana kwa mara ya kwanza mshambuliaji mashuhuri wa timu hiyo Marco Reus ambaye alikuwa nje tangu aliposhiriki katika mchezo wa fainali ya kombe la shirikisho nchini Ujerumani DFB Pokal mjini Berlin ambapo Borussia iliibuka mshindi kwa kuishinda Eintracht Frankfurt kwa mabao 2-1 mwezi wa May mwaka jana na kujikuta nje ya uwanja kwa kuwa majeruhi kwa muda mrefu.
Marco alionesha kwamba anahitajika sana katika kikosi hicho cha kocha Peter Stoeger ambacho kiishinda Hamburg SV kwa mabao 2-0 nyumbani. Huyu hapa Marco Reus.
"Hata mimi nimefurahi sana. Ni faraja kubwa kushiriki tena uwanjani. Nilifanyakazi kwa juhudi kubwa sana, ili niweze kurejea uwanjani. Hatukuonesha mchezo mzuri sana , lakini katika hali halisi, sijali sana, lakini pointi ni muhimu sana kwa sasa , ili tuweze kubakia katika nafasi za juu. Hamburg walitubana sana leo na kufanya kazi kuwa ngumu kwetu. Haikuwa bure kwamba walitoka sare ya bao 1-1 dhidi ya Leipzig wiki iliyopita."
Borussia Dortmund imesogea hadi nafasi ya tatu ikiwa na pointi 37, ikifuatiwa na Eintracht Frankfurt ambayo ina pointi 36, Bayer Leverkusen imeshuka kutoka nafasi ya pili wiki iliyopita hadi nafasi ya 5 ikiwa na pointi 35, ikifuatiwa na Schalke 04 na FC Augsburg katika nafasi ya 6 na TSG Hoffenheim baada ya kupata ushindi mnono wa kwanza katika mwaka huu wa 2018 wa mabao 4-2 dhidi ya Mainz 05 imetua katika nafasi ya 8. Huyu hapa kocha wa TSG Hoffenheim Julian Nagelsmann.
"Katika siku za nyuma kila mara tulikuwa tunapata upungufu, kwamba tunapata mabao machache kutokana na nafasi tunazopata na juhudi zetu tunazoweka. Na leo tulifunga kambi katika eneo la adui, tukipata mipira mingi inayorudishwa na walinzi wa timu pinzani na ndipo bao la kwanza la Andre lilivyopatikana. Wiki mbili zilizopita , nafikiri, hatungeweza kulazimisha mpira uingie wavuni. Lakini leo tumeweza, na nimefurahi sana kwa hilo."
Lakini hata hivyo pambano la kuvutia zaidi lilikuwa kati ya timu mbili zilizoko katika nafasi ya kushuka daraja. Werder Bremen katika nafasi ya 16 ilijitutumua na kutoka kifua mbele kwa kuizaba Wolfsburg kwa mabao 3-1, ikiikaribia timu hiyo iliyoko katika nafasi ya 13 sasa kwa tofauti ya bao moja.
Werder Bremen imetoka kutoka nafasi ya 16 sasa iko katika nafasi ya 15 pointi tatu juu ya Mainz 05 iliyoporomoka hadi nafasi ya 16. FC Kolon baada ya kichapo cha mabao 4-2 dhidi ya Eintracht Frankfurt imejichimbia bado mkiani mwa ligi ikiwa na pointi 13, ikifuatiwa na Hamburg SV ambayo nayo ina pointi 17 timu hizo zikipishana kwa pointi 4.
Mwandishi: Sekione Kitojo / dpae / afpe / rtre
Mhariri: Mohammed Khelef