Bayern Munich mabingwa mara tano
22 Mei 2017Bayern imetawazwa mabingwa kwa mara ya 27. Nahodha Philipp Lahm hata hivyo anatundika madaluga yake akiwa mchezaji wa kulipwa, akicheza mchezo wake wa mwisho akiwa mchezaji na nahodha wa Bayern kwa kuichapa Freiburg kwa mabao 4-1.
"Kwa wengi ilikuwa ni urafiki kwa miaka mingi.Tumeshuhudia mengi kwa pamoja. Kwa kweli inanisikitisha, kwamba hayo yote yanaondoka. Na kwangu mimi hilo lilinigusa sana wakati nikitoka uwanjani. Huo ulikuwa wakati mgumu sana kwangu."
RB Leipzig timu ambayo ilitoka daraja la pili msimu uliopita , hakuna mtu aliyeipa nafasi kwamba itafikia katika hatua ya kuchukua nafasi ya pili katika Bundesliga na kwamba itashiriki msimu ujao katika Champions League. Mvutano hata hivyo ulituwama katika kutafuta nani atachukua nafasi ya tatu ambayo ni ya kucheza moja kwa moja katika awamu ya makundi ya Champions League kati ya Hoffenheim na makamu bingwa msimu uliopita Borussia Dortmund. Ilibidi kusubiri hadi dakika za mwisho katika mchezo huo wa 34 wa Bundesliga kujua nafi ananyakua nafasi hiyo. Jibu lilipatikana baada ya Borussia Dortmund kuiangusha Werder Bremen kwa mabao 4-3 katika mchezo ambao ulikuwa wa vuta nikuvute, kama anavyothibitisha kocha wa Dortmund Thomas Tuchel.
"Vijana wanapaswa kujisikia furaha, na kwa kweli wamefanikiwa. Wamecheza vizuri msimu huu. Naamini kwa watu wote na klabu ulikuwa msimu mzuri na wa aina ya pekee. Na aina ya pekee huwezi kuieleza kwa jumla katika mistari miwili au mitatu."
FC Koln na Hertha Berlin zitashiriki msimu ujao katika kombe la ligi ya Ulaya , ambapo FC Koln wanaingia katika kinyang'anyiro cha Ulaya kwa mara ya kwanza katika muda wa miaka 24 iliyopita. SC Freiburg inaweza pia kuingia katika kinyang'anyiro cha kombe la ligi ya Ulaya iwapo , Borussia Dortmund itaishinda Eintracht Frankfurt katika kombe la shirikisho DFB Pokal tarehe 27 mwezi huu mjini Berlin. Mshindi wa kombe hilo huingia katika kombe la Champions League, lakini kwa kuwa Borussia tayari wameshafuzu kuingia katika kombe hilo, ikishinda timu iliyoshika nafasi ya 7 katika ligi inaingia katika kombe la ligi ya Ulaya katika nafasi ya mchujo.
FC Ingolstadt na Damstadt zimeaga ligi ya Bundesliga na msimu ujao zitashiriki ligi daraja la pili. Lakini kutoka ligi daraja la pili Stuttgart pamoja na Hannover 99 zinarejea katika Bundesliga msimu ujao, wakati Wolfsburg itacheza michezo miwili na Braunschweig iliyoshika nafasi ya tatu katika ligi daraja la pili ili kuamua nani anaingia katika ligi ya Bundesliga msimu ujao.
Bayer Leverkusen inatarajia kuwa na kocha mpya katika muda wa wiki chache zijazo akichukua nafasi ya Tayfun Korkut, amesema mkurugenzi mtendaji wa timu hiyo Michael Schade leo. Korkut alichukua nafasi ya Roger Schmidt mwezi Machi lakini mkataba wake haukurefushwa kupindukia msimu huu baada ya Leverkusen kumaliza ikiwa ya 12.
Mwanamke polisi mwezi umri wa miaka 38 Bibiana Steinhaus atakuwa mwanamke wa kwanza msimu ujao kuwa mwamuzi mwanamke katika ligi kubwa barani Ulaya baada ya kupandishwa kuweza kusimamia ligi ya Bundesliga.
Steinhaus amekuwa mwamuzi wa nne kwa akisimamia michezo ya Bundesliga na licha ya kuwa mwamuzi wa shirikisho la soka la Ujerumani DFB tangu mwaka 1999, na anatambua kwamba macho yatakuwa kwake kila mara wakati atakapokuwa mwamuzi wa mchezo mkubwa katika Bundesliga.
Mwandishi: Sekione Kitojo
Mhariri: Mohammed Khelef