Bayern Munich yachukua uongozi kutoka Schalke
5 Aprili 2010Bayern Munich, imerudi kileleni mwa Bundesliga, baada ya kuzima vishindo vya Schalke kwa mabao 2:1 Jumamosi.
Chelsea, kwa bao la Coast ,Didier Drogba , iliizaba nayo manchester united pia kwa mabao 2:1.
Simba ya Tanzania, yatamba katika Kombe la Shirikisho la dimba la Africa-Confederation Cup.
Na Afrika Kusini, imeteleza katika maandalio yake ya Kombe lijalo la dunia kwa kulazwa jana na timu ya akiba ya klabu ya zamani ya Pele,Santos.
Tangu katika Bundesliga hata Premier League, mwishoni mwa wiki, ilikua changamoto kati ya timu ya kwanza kileleni na ile ya pili:Schalke na Bayern Munich na Chelsea na Manchester United:
Ni Frank Ribery na Thomas Mueller, waliolifumania lango la Schalke kwa mabao 2 ya Bayern Munich katika kipindi cha kwanza.
Ikionekana kana kwamba, Schalke imeshakata roho, Kevin Kuranyi, aliifufua Schalke kwa bao lake dakika 5 tu baada ya bao la Mueller. Schalke ikaanza kulihujumu lango la Bayern Munich ambayo kwa kutolewa nje ya chaki ya uwanja kwa Hamit Alintop , Bayern munich ilijikuta inacheza na wachezaji 10.Hatahivyo, vishindo vya wenyeji Schalke, havikufua dafu.Kwani, Munich, mwishoe, iliondoka na pointi zote 3 na sasa imeunyakua usukani wa Bundesliga kutoka mikononi mwa schalke.Munich, lakini, inaongoza kwa pointi 1 , ikifuatwa nyuma na Schalke na Bayer Leverkusen.Mwishoni mwa mpambano huo, kocha wa Bayern Munich, Van gaal alisema:
"Ulikuwa mpambano mgumu.Kwa bahati nzuri tulitia mabao 2 na nadhani ushindi wetu ulistahiki mno."Leverkusen, ilioongoza Bundesliga, mapambano 24 bila kushindwa , sasa inapepesuka .Mwishoni mwa wiki, Leverkusen, ilikandikwa mabao 3-2 na Frankfurt na imeangukia nafasi ya 3.Dortmund,imen'gan'gania nafasi ya 4 na sasa iko pointi 1 tu nyuma ya Leverkusen.
Hertha Berlin, inayoburura mkia wa Bundesliga, yaonesha imejizatiti kuachana na mkia huo.Kwani, ilitamba tena hapo Jumamosi, ilipoizaba FC Cologne, nyumbani mwake mabao 3:0.Stuttgart imeikamata kwa pointi Hamburg baada ya kuishinda Borussia Moenchengladbach kwa mabao 2:1.Nuremberg ikatamba kwa mabao 2:0 dhidi ya Mainz.
Hamburg jana , haikumudu zaidi ya sare na Hannover.Changamoto iliokamilisha kalenda ya Bundesliga mwishoni mwa wiki, ilikua kati ya mabingwa Wolfsburg na Hoffenheim.Wolfsburg ikatamba kwa mabao 4:0.
Kocha wa Wolfsburg,Köstner , akiipongeza timu yake alisema:
"Leo tumepata bahati ya kutotiwa kwanza bao .Na tulipotia bao, tulijua kuwa tuna wachezaji ambao wana uwezo wa kuamua mchezo. "
Ama katika pirika-pirika za kuania uongozi wa Premier League-ligi ya Uingereza,Chelsea, imekuja juu ya Manchester United.Bao la Muivory Coast, Didier Drogba, lilitosha kuzima vishindo vya Manu na kuipa pigo la pili kali baada ya lile la kati ya wiki kutoka Bayern Munich katika champions league-kombe la klabu bingwa barani ulaya. Alikuwa Joe Cole, aliepiga hodi kwanza katika lango la Manu na kukaribishwa ndani.Bao la Manu lilitiwa na mchezaji wa akiba Frederico Macheda na halikuwa zaidi ya kuifuta machozi Manchester. Berbatov, aliejaza pengo la wayne Rooney, alieumia, alipata nafasi ya kusawazisha, lakini hakufua dafu.
Kocha wa Chelsea, Carlo Ancelotti,anadai sasa kwamba, Chelsea, ndio itakayo toroka na taji la Premier League msimu huu. Manu inaikumbusha Chelsea, kwamba ,iliwahi kutangulia,lakini bado haikufika.Arsenal, yaonesha impoteza nafasi ya kujaza pengo kati ya Chelsea na Manu.Kwani, ilimudu suluhu tu ya 0:0 na Wolvehampton Wanderes.
Wakati hali ya usalama nchini Afrika Kusini,imechafuliwa kwa kuuwawa kwa kiongozi wa kikaburu mwenye siasa kali ,Bafana Bafana ikijiandaa kwa kombe lijalo la dunia nchini Brazil, ilipatwa nayo na msukosuko ilipolazwa jana na timu ya wachezaji wa akiba wa klabu ya Santos, klabu ya zamani ya Pele.Santos iliifunga Afrika Kusini mabao 2:1.
Kocha wa Afrika Kusini, mbrazil, Carlos Parreira ,aliongoza mazowezi ya wiki 3 huko Brazil ili kuiandaa Afrika kusini, kukabili vishindo vya Kombe la dunia hapo Juni,mwaka huu. Jumatano iliopita, Afrika kusini, ilitoka sare na Paraguay kwa kuchapana bao 1:1.
Afrika kusini, ndio itakayofungua dimba Juni 11 mwaka huu, na Mexico huko City Stadium, mjini Johannesberg. Ufaransa na Uruguay, ni timu nyengine 2 ambazo ziko kundi moja na Bafana Bafana.
Katika kinyan'ganyiro cha Kombe la klabu bingwa barani Afrika, JS Kabylie ya Algeria, imeitoa Club Africain ya Tunisia kwa bao 1:0 na kufuatia ushindi wa duru ya kwanza, waalgeria sasa wanasonga mbele duru ijayo kwa jumla ya mabao 2:1.
Mwandishi:Ramadhan Ali/Agenturen
Mpitiaji:Mohammed Abdul-Rahman