1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

BAYERN MUNICH YAICHAPA DORTMUND 5:0

21 Februari 2005

BAYERN MUNICH YAIZABA BORUSSIA DORTMUND MABAO 5-1 KATIKA BUNDESLIGA

KOMBE LA KLABU BINGWA BARANI AFRIKA

NA MJI WA LONDON UKO NYUMA YA MJI WA PARIS KATIKA KINYAN’GANYIRO CHA KUANDAA OLIMPIK 2012

Baada ya Bayern munich kuirarua Borussia Dortmund jumamosi kwa mabao 5-0,jana ilikua zamu ya Schalke kuilaza Borussia Mönchengladbach mabao 3:1.Mabao yote ya Schalke yalitiwa na mbrazil Ailton.Ilikua lakini Mönchengladbach iliotangulia kuufumani mlango wa Schalke kwa mkwaju wa penalty aliouchapa Joerg Boehme.

Ushindi huo umeipa schalke jumla ya pointi 44 kutoka mechi 22 sawa na viongozi wa Ligi Bayern Munich.

Hapo jumamosi iliobainika kila kitu kinaiendea kombo Borussia Dortmund,kwani mbali ya msukosuko wa fedha unaoijongeza klabu hii kufilisika, ilizabwa mabao 5:0 na bayern Munich na huo ukawa kupiga msumari juu ya donda.

Borussia Dortmund inakabiliwa na deni la hadi dala milioni 175.3.Ni mwaka 2001 tu ambapo klabu hii iliibuka mabingwa wa Ujerumani baada ya kutawazwa mabingwa wa ulaya 1997.

Mholanzi Roy Makaay alipiga hodi mara tatu katika lango la Borussia Dortmund na kukaribishwa ndani-Hattrick.Ni mwishoni mwa wiki iliotangulia ambapo bayern Munich ilikandikwa mabao 3:1 na Armenia Bielefeld.

Nahodha wa Ujerumani Michael ballack yamkini akakosa kuichezea Bayern Munich kesho itakapoteremka uwanjani katika dimba la Kombe la Ulaya kati yake na Arsenal London.Bayern Munich ilicheza jumamosi bila Ballack.

Mabingwa Werder Bremen sasa wamewasili nafasi ya tatu ya ngazi ya Ligi wakiwa na pointi 40.Bremen ilikumta Hannover 96 mabao 4:1.

Bayer Leverkusen ambayo kesho ina midai katika champions League-Kombe la klabu bingwa barani Ulaya, iko nafasi ya 4 ikiwa na pointi 38.Leverrkusen iliitandika Nüremberg mabao 4-2.Stuttgart inajikuta sasa nafasi ya 5.

Nahodha wa zamani watimu ya taifa ya Misri Hany Ramzy anaanza leo kazi ya kusomea ukocha baada ya kuridhia kwamba klabu yake ya Kaiaserslauten haitamchezesha tena katika Bundesliga.

Ramzy mwenye umri wa miaka 35 alieumia tangu August 2003,hakuondoa uwezekano wa kurejea kucheza lakini hataweza kufanya hivyo kabla mkataba wake na Kaiserslauten kumalizika mwisho wa msimu huu.

Hany Ramzy ameichezea Misri mara 124 na mara 2228 kwa Kaiserslauten.

Katika changamoto za jana za Kombe la klabu bingwa barani Afrika,Rayon sport ya rwanda iliilaza Motema Pembe ya Jamhuri ya kidemokrasi ya kongo kwa mabao 2:0.Mjini Nampula,Ferroviario Nampula ya Msumbiji ilitoka suluhu 1:1 na Simba ya Tanzania.Mjini Zanzibar,KMKM ilizabwa mabao 3:0 na Tusker ya Kenya.

Sasa Simba ya Tanzania itakumbana na Enyimba katika duru ijayo.

Makame Abdullah anasimulia sasa kutoka Zanzibar uwezekano wa Zanzibar kuandaa Kombe la vijana la chini ya umri wa miaka 19 kanda ya CECAFA:

Katika kinyan’ganyiro cha kuania mji gani utaandaa olimpik 2012, ni zamu ya jiji la New York kujitembeza.Uchunguzi umeonesha kwamba, jiji la London liko nyuma ya Paris katika kinyan’ganyiro hiki.

Licha ya matumaini yalioibuka wakati wa ziara ya Tume ya IOC-Halmashauri kuu ya olimpik ulimwenguni mjini London,imeonekana kwamba,mji wa London ungali uko nyuma ya jiji la Paris litakalotembelewa na Tume hiyo hapo Machi 9.

Tume ya IOC inayotathmini zana za miji inayogombea iko sasa mjini New York,Marekani baada ya ziara yxake ya london na Madrid.

Baadae itaelekea Paris na Moscow mwezi ujao.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW