Bayern Munich yaisubiri Real Madrid
23 Aprili 2018Champions League inarejea uwanjani tena kesho na keshokutwa Jumatano katika awamu ya nusu fainali, ambapo klabu kutoka ligi nne kubwa za Ulaya zinawakilishwa. Kwa mara ya kwanza tangu mwaka 1981, timu kutoka Uhispania , Real Madrid England Liverpool, Italia Roma na Ujerumani Bayern Munich zinakuwa timu nne za mwisho katika kinyang'anyiro hicho cha juu cha vilabu barani Ulaya.
Roma inasafiri kwenda mjini Liverpool kwa mkondo wa kwanza wa nusu fainali ya Champions League, wakitarajia kupata matokeo mazuri ambayo yalianzia katika kuitupilia mbali Barcelona. Kocha wa Roma Eusebio Di Francesco anakichukua kikosi chake kwenda Liverpool kesho Jumanne katika mchezo huo wa kwanza.
Di Francesco , aliyechukua nafasio ya Luciano Spalletti Juni mwaka jana, alikuwa kijana mwaka 1984 wakati Liverpool ilipoigaragara Roma nyumbani katika fainali ya kombe la Ulaya, kama lililvyokuwa linafahamika wakati huo.
Liverpool ilinyakua taji lake la nne kati ya mataji matano ya bara la Ulaya kwa kupigiana penalti baada ya kutoka sare kwa bao 1-1 katika uwanja wa Stadio Olimpico.
Miaka 17 baadaye Di Francesco alikuwa katika benchi la Giallorossi akiwa mchezaji wa kiungo akiwaangalia Liverpool wakishinda kwa mara nyingine tena kwa jumla ya mabao 2-1, katika timu 16 zilizobakia katika kombe la UEFA mwaka 2001.
Lakini siku ya Jumatano kutakuwa na patashika nyingine ya nusu fainali, wakati bayern Munich ikicheza nyumbani katika mchezo wa mkondo wa kwanza , ina malengo ya kulipiza kisasi cha kufungwa msimu uliopita na Real Madrid katika michezo yote miwili katika robo fainali.
Bayern Munich imekuwa na matatizo na timu za Uhispania hivi karibuni na kuondolewa mashindanoni katika misimu minne mfululizo dhidi ya timu za Uhispania. Bayern iliondolewa mashindanoni na Real mwaka 2014, Atletico Madrid mwaka 2015 na barcelona 2016. Mwaka jana Real iliiondoa Bayern katika robo fainali. Real Madrid inawania kulibeba kombe hilo kwa mara ya tatu mfululizo.
Mwandishi: Sekione Kitojo / dpae / afpe / rtre
Mhariri: Yusuf , Saumu