1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Shirika la haki za binadamu laitupia lawama Bayern Munich

31 Agosti 2023

Shirika la Haki za Kibinadamu la Human Rights Watch limekosoa mpango mpya wa ushirikiano kati ya serikali ya Rwanda na Bayern Munich

Deutschland | Pressekonferenz FC Bayern München
Mkurugenzi Mtendaji wa Bayern Munich Jan-Christian Dreesen ameeleza kwamba ushirikiano huo mpya unaonyesha alama mpya na ya kwanza kwa Bayern barani AfrikaPicha: Sven Hoppe/dpa/picture alliance

   

Klabu ya Bayern Munich imekosolewa na shirika la Haki za Kibinadamu la Human Rights Watch (HRW) kuhusu ushirikiano wake na nchi ya Rwanda katika mpango wa maendeleo ya soka na kukuza utalii nchini Rwanda.

Soma zaidi: Bayern Munich yamruhusu Pavard kwenda Inter Milan

Siku ya Jumapili klabu hiyo ilitangaza kuingia makubaliano ya ushirikiano wa maendeleo ya soka kwa miaka mitano kwa kutangaza kampeni ya utalii ya "Visit Rwanda " yenye lengo la kuwahamasisha watalii kote ulimwenguni kuitembelea nchi hiyo ya Afrika ya Mashariki.

Mkataba huo umekuja baada ya Bayern Munich kutoendelea na Qatar Airways ambayo pia ulikosolewa na makundi ya haki za binadamu pamoja na mashabiki wa klabu hiyo.

Mchezaji mpya wa Bayern Munich Harry Kane akishangiilia goli katika mechi yake ya kwanza dhidi ya Werder BremenPicha: Ina Fassbender/AFP/Getty Images

Mkurugenzi Mtendaji wa shirika hilo hapa Ujerumani Wenzel Michalsk amesema "Yeyote ambaye alifikiria kuwa Bayern wanabadilisha mfadhili kwa sababu za kiutu atakuwa amekatishwa tamaa''

Mkurugenzi huyo ameongeza kuwa "Ushirikiano wa sasa na Rwanda ni chaguo baya sana''

"Ni nchi  ambayo haki za binadamu zinakanyagwa," Michalski alisema.

Rwanda inayoongozwa na rais Kagame inatajwa kuwa ni nchi ambayo watu wanaoipinga serikali yake wanachukuliwa kuwa ni tishio kwa nchi hiyo na kwamba hakuna uhuru wa watu wanaokinzana na serikali yake.

Soma zaidi: Kane asema atahitaji muda wa kuzoea kandanda la Ujerumani

Ripoti ya Amnesty International inasema: "Kuna ukiukwaji wa haki, uhuru wa kujieleza na uhuru wa faragha ambao bado unaendelea,  sambamba na kupotea kwa watu, madai ya utekaji na matumizi ya kupita kiasi ya
nguvu."

Mkurugenzi Mtendaji wa Bayern Munich Jan-Christian Dreesen ameeleza kwamba ushirikiano huo mpya unaonyesha alama mpya na ya kwanza kwa Bayern barani Afrika na kwamba hizi ni changamoto na tunawajibika kwa namna yake ila kwa sasa Afrika ni bara la fursa na  FC Bayern, hii ni hatua inayofuata muhimu katika utangazaji wa kimataifa.


Clare Akamanzi, Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi ya Maendeleo ya Rwanda, amesema kuwa ''ushirikiano na Bayern "unaturuhusu kufikia mamilioni yake ya mashabiki kote ulimwenguni na kuwaambia kuwa watembelee Rwanda''