Bayern Munich yamkaribisha Pep Guardiola
25 Juni 2013Guardiola amesema leo kuwa aliamua kujiunga na washindi hao wa mataji matatu msimu huu kwa sababu ya wachezaji na historia ya kujivunia ya klabu hiyo. Mhispania huyo mwenye umri wa miaka 42, amewaambia waandishi wa habari kwamba alihitaji changamoto mpya baada ya misimu minne yenye mafanikio kama kocha wa Barcelona kipindi ambacho alishinda mataji 14, ikiwa ni pamoja na mataji mawili ya Champions League, kati ya mwaka wa 2008 – 2012. kisha akaamua kupumzika kwa mwaka mmoja jijini New York pamoja na familia yake ambako alianza kujifunza Kijerumani na akasaini mkataba wa miaka mitatu na Bayern, ambao walinyakua taji la Bundesliga, Kombe la Shirikisho pamoja na Champions League chini ya Jupp Heynckes katika msimu uliopita.
Pep azungumza Kijerumani
Guadiola alianza kwa kusema na namnukuu, “niwie radhi kwa kijerumani changu, New York siyo sehemu nzuri ya kujifunza Kijerumani”. Akizungumza katika lugha ya Kijerumani, Kocha huyo amesema anahisi kama amepewa zawadi na ana furaha kujiunga na Bayern.
Amesema yuko tayari kufanya kila awezalo kuendeleza mafanikio ya klabu ya Bayern kwa kuiweka katika kiwango cha juu alichoweka mtangulizi wake Jupp Heynckes.
Mwenyekiti wa klabu hiyo Karl-Heinz Rummenige amesema ni bahati, fahari na mafanikio kumpata kocha mwenye ufansi kote ulimwenguni. Kwamba pande zote zilitaka hilo: Bayern ilimtaka Pep, na Pep akaitaka Bayern. Hivyo ni hadhithi ya kusisimua ya Bayern Munich na soka ya Ujerumani.
Matarajio yako juu. Bayern wamehamishia mazoezi yao ya siku mbili chini ya Guardiola katika uwanja wa Allianz Arena huku takribani mashabiki 25,000 wakitarajiwa kushuhudia. Mengi yameandikwa kuhusiana na filosofia ya mchezo wa kasi wa Tiki Taka ambao Barcelona waliutawala chini ya Mhispania huyo, lakini itasubiriwa kuona kama atahama kutoka muundo wa 4-2-3-1 hadi 4-3-3.
Mwandishi: Bruce Amani/reuters/DPA
Mhariri: Yusuf Saumu