Bayern Munich yamtaka Miroslav Klose wakati Real Madrid Beckham
11 Juni 2007Bayern Munich imeshatumia Euro milioni 36 kuwanunua mastadi wawili:Frank Ribery kutoka Ufaransa na Lucatoni kutoka mabingwa wa dunia Itali.Sasa Munich inamtaka mtiaji mabao mengi katika kombe lililopita la dunia Miroslav Klose kutoka Werder Bremen.Bremen haibishi kumuachia Klose kujiunga na B.Munich,lakini inadai ipatiwe Lucas Podolski.Hii inakumbusha mabadilishano sawa na hayo miaka michache nyuma pale mlinzi wa Bremen,mfaransa Valery Ismael alipokwenda B.Munich na Frings akarejea Bremen.
Ruanda itakua tena mwenyeji wa kinyan’ganyiro cha kuania tiketi ya kombe la Afrika la mataifa huko Ghana mwakani kwa kuandaa tena changamoto kati ya Burundi na mabingwa Misri.Hii ni kwasababu uwanja wao waburundihauwezi bado kutumika.
Burundi ina miadi na Misri Juni 17 katika mpambano muhimu wa kundi la pili.Uwanja wa Burundi mjini Bujumba,umezuwiliwa kuchezewa mechi huku ukipatiwa busati la kisasa lisilo la majani la kuchezea dimba-artificial pitch.Burundi iliizaba Botswana bao 1-0 mjini Kigali hapo juni 3 na hii ikaipatia Burundi pointi 6,pointi mbili tu nyuma ya viongozi wa kundi hili Misri.
Taifa Stars ya Tanzania baada ya kumudu suluhu ya bao 1:1 na Senegal huko Mwanza hivi majuzi, ilijiwinda mwishoni mwa wiki ilipopimana nguvu na jirani zao Zambia mjini Morogorro,lakini baada ya kuongoza kwa bao 1,mwishoe,ilifanya madhambi yale yale na kuiachia Zambia kusawazisha 1:1 .
Nje ya Afrika Mashariki, Enyimba wameibuka mabingwa wapya wa Nigeria baada ya kumudu jana suluhu ya bao 1:1 na Gombe United.Ilikua Gombe lakini iliowasangaza Enyimba ilipotia bao kwanza mnamo dakika ya 32 ya mchezo, lakini Enyimba ikawambia kutangulia sio kufika.dakika 9 zikisalia kabla ya firimbi ya mwisho kulia, Uche Kalu alisawazisha na kuipatia Enyimba ubingwa wa Nigeria kwa mara ya 5.
Wanariadha wa Afrika mashariki na kati walitamba katika mashindano ya riadha ya Grand Prix huko Eugene,Oregon,Marekani.
Katika mita 400 mkongomani Gary Kikaya aliwapiku majogon wa Marekani kwa muda wake wa sek 44.93 huko Lashawn na Angelo Taylor wa Marekani:
Katika mbio za maili 1 ,Daniel Kipchichir Komen wa Kenya alimpiku Bernard Lagat,Muamerika mzaliwa wa Kenya na kuchukua ushindi.Watatu alifuata mkenya mwengine Alex Kipchirchir.
Ama katika zahama ya maili 2 Muethiopia Tariku Bekele alibidi kuridhika na nafasi ya pili huku ushindi ukienda kwa Muastralia Craig Mottram.
Katika mbio za mita 3000 kuruka viunzi-steeplechase-Paul Kipsiele Koech alitamba na kuipatia Kenya ushindi.
Upande wa wasichana,Maria Mutola wa Msumbiji alinyakua ushindi katika mita 800 akimtupa nafasi ya pili Kenia Sinclair wa Jamaica na Alice Schmidt wa Marekani akibidi kuridhika na nafasi ya tatu.
Kwenye changamoto ya mita 1500,Gelete Burka wa Ethiopia alitoroka na ushindi.