Bayern Munich yashindwa kumaliza kazi ya ubingwa
13 Mei 2019Mvutano kama uliotokea katika Premier League unaonekana kujitokeza pia katika Bundesliga msimu huu. Bayern Munich inaongoza msimamo wa ligi kwa kuwa na pointi 75 , wakati hasimu wake wa karibu Borussia Dortmund ina pointi 73.
Ni mchezo wa mwisho wa 34 utakaoamua nani anabeba ngao ya ubingwa katika Bundesliga msimu huu. Iwapo Bayern itaondoka na ushindi, ikihitaji sare tu kunyakua ngao hiyo kwa mara ya saba mfululizo, hilo ni suala la kusubiri na kuona. Bayern Munich itakuwa nyumbani katika mchezo wake huo ikiwakaribisha Eintracht Frankfurt, wakati Borussia Dortmund itakuwa ugenini ikipambana na Borussia Moenchengladbach.
Bayern Ilishindwa mwishoni mwa juma kukamilisha ubingwa wake wa saba baada ya kutoka sare ya bila kufungana na RB Leipzig katika uwanja wa Red Bull Arena siku ya Jumamosi.
Hata hivyo wachambuzi wanaona hakutakuwa na kazi kubwa kwa Bayern kukamilisha ubingwa wake wa saba mfululizo itakapokumbana na Frankfurt ambayo baada ya kutolewa katika mchezo wa nusu fainali ya Europa League kwa mikwaju ya penalti dhidi ya Chelsea ya Uingereza, nguvu zimewaishia na hawatakuwa na ubavu wa kuizuwia Bayern kunyakua taji lake hilo la saba. Lakini mpira unadunda na kila kitu kinawezekana. Na hapo ndio matumaini ya Borussia Dortmund yanapojikita.
Frankfurt ilitandikwa mabao 2-0 jana jumapili na Mainz 05 katika mchezo wa mwisho wa kukamilisha duru ya 33 ya Bundesliga.