Bayern yatunisha misuli katika Bundesliga
10 Aprili 2017Ulikuwa mwisho wa juma wa kilio na masikitiko makubwa kwa makamu bingwa wa ligi ya Ujerumani Bundesliga Borussia Dortmund baada ya kugaragazwa na mabingwa watetezi wa ligi hiyo Bayern Munich siku ya Jumamosi kwa kukandikwa mabao 4-1 katika uwanja wa Allianz Arena mjini Munich. Bayern inaongoza ligi hiyo kwa pointi 10 kutoka timu inayoifuatia RB Leipzig , wakati timu ya tatu inayoifuatia Bayern ni TSG Hoffenheim na Borussia Dortmund ikiwa katika nafasi ya nne. Kocha wa bayern Carlo Ancelotti baada ya mchezo huo alisema tu kwamba kila kitu kilikuwa sawa na sasa tunaisubiri Real Madrid katika mchezo wa Champions League hapo Jumatano.
Nae mshambuliaji wa Bayern Munich Arjen Robben ambaye aliisumbua sana safu ya ulinzi ya Dortmund na hatimaye kutia saini yake kwa bao safi la 3 alikuwa na haya ya kusema .
"Ulikuwa mchezo mzuri sana. Unakuwa ndani ya mchezo huo, na kuonekana. Nijisikia raha sana. Mimi si kijana tena, na ninapaswa kufurahia mchezo. Leo kila kitu kilikuwa kizuri."
Kwa bao la dakika za mwisho RB Leipzig , sio tu ilishinda mchezo wake dhidi ya Bayer 04 Leverkusen kwa bao 1.0 lakini pia imeimarisha nafasi yake ya kufuzu moja kwa moja kucheza katika ligi ya mabingwa barani Ulaya Champions League msimu ujao , ikiwa ni timu iliyotokea daraja la pili msimu huu. Kocha wa Leipzig Ralph Hasenhüttel anathibitisha hilo.
"Naam , hii ndio sababu ya sisi kuja hapa uwanjani. Kwasababu tunataka kushuhudia mchezo kama huu, kama kocha, timu na pia mashabiki. Hizi ndio hisia za kandanda. Mna mchezaji mmoja pungufu uwanjani na mnashinda na hasa katika dakika za mwisho. Huu ni wakati , maalum wenye utamu wa aina yake. Kwetu sisi ilikuwa siku ya ushindi muhimu sana."
FC Kolon kwa mara nyingine tena imeteleza mbele ya adui yake anayemuogopa kila mara. Kolon imeshindwa kutamba nyumbani kwa kukandikwa mabao 3-2 na Borussia Moenchengladbach katika Derby ya eneo la mto Rhine siku ya jumamosi, ushindi ulioisukuma timu hiyo kuikaribia Kolon kwa kutofautiana nayo kwa pointi moja tu katika nafasi ya nane , wakati Kolon iko nafasi ya saba katika msimamo wa ligi ya Bundesliga msimu huu, na kuporomoka kutoka nafasi ya kucheza katika ligi ya Ulaya msimu ujao.
Kocha wa Gladbach Dieter Hecking amesema timu yake ilikuwa na nia ya ushindi tangu mwanzo.
"Uliweza kuona kuanzia dakika ya mwanzo , kwamba tulitaka kushinda. Tulitaka kushinda, bila kujali vile Kolon inavyoweza kuhimili. Tulitaka kila wakati kuonesha , kwamba kidogo uwezo wetu ni mkubwa , ambao unatuwezesha kushinda. Hilo timu yangu ililifanya vizuri."
Hamburg SV kwa mara ya tatu mfululizo imeweza kushinda mchezo wake wa nyumbani kwa kuiangusha 1899 TSG Hoffenheim kwa mabao 2-1 na kujikongoja kidogo kidogo kutoka katika eneo la hatari ya kushuka daraja , licha ya kwamba kitisho hicho hakijamalizika.
Schalke 04 nayo ikaonesha kwamba uwezo wake unadhoofishwa msimu huu na matatizo ya wachezaji wake wengi kuwa majeruhi , kwa kuicharaza VFL Wolfsburg kwa mabao 4-1 , wakati Hertha Berlin iliishinda Augsburg na kuisababishia timu hiyo kuingia katika hofu ya kushuka daraja.
Augsburg iko sasa katika nafasi ya 16, ikiwa pamoja na FC Ingolstadt na Damstadt ikishika mkia. Njia ya damstadt kuelekea daraja la pili iko nyeupe baada ya jana Jumapili kukandikwa mabao 3-2 na Ingolstadt ambayo inajaribu kujinasua kutoka hatari ya kushuka daraja , ikiwa na pointi 28 , moja tu chini ya Augsburg , na FSV Mainz zote zikiwa na pointi 29. Lakini pia VFL Wolfsburg yenye pointi 30 haiko salama sana.
Mwandishi: Sekione Kitojo / afpe / APE
Mhariri:Iddi Ssessanga