1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Bayern Munich

6 Oktoba 2008

Munich haitishi tena katika Bundesliga-Beckenbauer.

Franz Beckenbauer,adai timu za Bundesliga hazina tena heshima mbele ya mabingwa Bayern Munich.Borussia Młnchengladbach,yamtimua kocha wake Jos Luhukay baada ya FC Cologne kuizaba 2:1.Mkenya. Sammy Kurgat ashinda ashinda Cologne -marathon kwa muda wa rekodi wa mbio hizo na tutawachukua kusikia mapya katika viwanja vya michezo kanda ya Afrika mashariki:

LIGI MASHUHURI ZA ULAYA:

Katika Bundesliga-ligi ya Ujerumani, ni Hamburg ilio kileleni na sio Bayern Munich kama ilivyo desturi.Wakati mabingwa walimudu suluhu ya mabao 3:3 na Bochum baada ya kuongoza kwa mabao 3:1 ,Hamburg imetoroka na pointi zote 3 jana baada ya kuikomea Energie Cottbus kwa mabao 2-1.

Bao la dakika ya 54 la Ivica Olic lilifutwa na Branko Jelic dakika 20 baadae hata hivyo, Hamburg ikatoroka na ushindi pale mcroatia mwengine Mladen Petric alipolifumania lango la Cottbus kwa kichwa dakika ya 90 ya mchezo na kuondoka na ushindi.

Schalke iliweza dakika ya mwisho kusawazisha katika mpambano wake na Wolfsburg uliomalizika kwa sare ya mabao 2:2.Borussia Dortmund ilimudu pia sare ya bao 1:1 na Hannover wakati Stuttgart ilitamba mbele ya Bremen kwa mabao 4:1.Hoffenheim ikaizaba Eintracht Frankfurt 2-1.

Katika kindumbwe-ndumbwe kati ya mahasimu wakubwa wa jadi-FC Cologne na Borussia Monchengladbach,FC Cologne ilitamba nyumbani mwa Borussia na kuondoka na ushindi wa mabao 2:1.Pigo hili liliisukuma Borussia Monchengladbach mkiani mwa Bundesliga na hivyo uongozi wa Gladbach ukaamua kumtimua nje kocha wao Jos Luhukay.Borussia imefungwa mechi 6 kati ya 7 za msimu huu mpya na hivyo jumamosi maji yalizidi unga.

Borussia Monchengladbach ikatangaza kwamba ,mkurugenzi wake wa spoti Christian Ziege anachukua usukani kwa muda.Ziege ni mchezaji wa zamani wa taifa.Borussia iliteremshwa daraja ya pili 2007 kwa mara ya pili,lakini alikuwa kocha Jos Luhukay alieipandisha tena daraja ya kwanza.

Wakati hatima ya kocha Jos Luuhukay sasa inajulikana, ile ya kocha maarufu Jurgen klinsmann wa klabu bingwa Bayern munich haijulikani.Munich iliteleza tena jumamosi ilipoongoza kwa mabao 3:1 na mwishoe, Bochum ikatoka nyuma na kusawazisha na kufanya mabao 3:3.

Baada ya pigo hilo, kocha Klinsmann alisema:

"Matokeo kwa jicho letu si ya kuridhisha.Ukiongoza kwa mabao 3:1 na ukiwa umepata nafasi za kutosha kutia la 4 na hata la 5,huachii mchezo ukakuponyoka.Hii inakera sana lakini hatuwezi kubadili."

Nahodha na rais wa zamani wa Bayern Munich, Franz Beckenbauer,akichambua hali inayojikuta klabu yake ,alisema timu za Bundesliga zimepoteza heshima za kuiogopa Bayern Munich kwamba haishindiki. Kwani, timu ndogo haziheshimu tena Bayern Munich-alisema Beckenbauer.Utakumbuka kwamba Munich kabla kumudu sare mwishoni mwa wiki ya mabao 3:3 na Bochum, ilitoka sare 2 na kushindwa mara 2.

Ama katika Premier League -Ligi ya Uingereza, FC Liverpool ilitoka nyuma jana na i na mwishoe, ikaondoka na ushindi wa mabao 3-2 dhidi ya Manchester City.Kwa ushindi huo Liverpool, imeshika uongozi kilelelni pamoja na Chelsea iliotamba mbele ya Aston Villa kwa mabao 2:0.Matokeo hayo maana yake timu zote 2 zina pointi 17-pointi 3 mbele kuliko Hull City,ilioendelea na ushindi wake wa kusangaza kwa ushindi wa bao 1:0 dhidi ya Tottenham Hotspur.Mabao ya kipindi cha kwanza ya Joe Cole na Nicolas Anelika yaliifanya Chelsea kutamba mbele ya Aston villa.

Katika changamoto za La Liga huko Spian, Valencia wamerudi kileleni kufuatia ushindi wao wa bao 1:0 mbele ya Valladolid. Bao maridadi ajabu alilotia Manuel fernandes mnamo dakika ya 55 ya mchezo,lilitosha kuizika Valladolid.

Baadae jana,Real Madrid walizimwa sare ya mabao 2-2 tena nyumbani na Espanyol walioongoza mara 2.Barcelona na Real wako pointi 1 nyuma ya Sevilla walioizaba athletico Bilbao mabao 4-0.

Serie A,Ligi ya Itali -Napoli imekosa nafasi ya kuparamia kileleni mwa ngazi ya Ligi hapo jana kwani wenyeji Genoa, walitamba kwa mabao 3-2.Hatahivyo, Napoli iko pointi 2 nyuma ya viongozi Lazio,Udinese na mabingwa Inter Milan.

COLOGNE-MARATHON

Kama desturi yao, wakenya wametamba tena mwaka huu katika mbio za Cologne-marathon hapo jana: Mkenya Sammy Kurgat alishinda kwa kuivunja rekodi ya miaka 4 iliopita ya Cologne marathon iliowekwa na mkenya mwenzake James Rotich kwa muda wa sekunde 21.Muda wa ushindi wa Kurgat ulikuwa masaa 2:10:01-rekodi mpya.

Upande wa wanawake, ushindi ulikwenda kwa msichana wa Ethiopia Robe Tola Guta.Robe alichukua muda wa masaa 2:29:36. Robe alimkimbia mjerumani Luminita Zaituc muda mfupi kabla kumaliza mbio hizo.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW