1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Bayern na Dortmund dimbani fainali ya DFL Super Cup

28 Septemba 2020

Miamba ya kandanda ya Ujerumani Bayern Munich na Borussia Dortmund iliangukia pia mwishoni mwa wiki katika mechi zao za ligi kuu Bundesliga lakini wana fursa ya kurejea tena haraka kwenye mkondo wa ushindi.

Bundesliga - Borussia Dortmund v Bayern München
Picha: REUTERS

Itakutana kwa mara ya kwanza msimu huu siku ya Jumatano dimbani Allianz Arena katika fainali ya DFL Super Cup. Washindi wa mataji mawili makuu ya nyumbani Bayern watawaalika Dortmund ambao ni makamu bingwa wa Bundesliga, kujaribu kubeba taji lao la tano katika mwaka wa 2020.

Baada ya mechi 32 za ushindani bila kushindwa, ukiwemo ushindi wa mechi 23 za mwisho, Bayern walionja kichapo kizito jana cha 4 – 1 mikononi mwa Hoffenheim. Walicheza saa 48 tu baada ya kurejea kutoka Budapest, ambako walibeba taji lao la nne katika mwaka mmoja la UEFA Super Cup dhidi ya Sevilla, ushindi uliopatikana katika muda wa nyogeza.

Hoffenheim waliwazidi Bayern maarifaPicha: Wolfgang Rattay/Reuters

Kocha wa Bayern Munich Hansi Flick amekataa kutoa sababu ya uchovu wala kuwalaumu wachezaji wake kwa kipigo hicho maoni ambayo yanaungwa mkono na Thomas Müller. Ni wazi kuwa ingefika siku ambayo unapoteza mechi nyingine. Nadhani tulikuwa pia na nafasi moja au mbili ambazo tungeweza kurekebisha. Lakini kwa dakika 90 hatukustahili kutoka sare au hata kushinda mchezo. Hoffenheim ilifanya kazi nzuri leo. Kwa mukhtasari, tulistahili kushindwa na tutarudi Jumatano.

Hoffenheim wanaongoza kwa sasa msimamo wa ligi lakini Kocha Sebastian Hoeness, ambaye ni mpwa wa rais wa heshima wa Bayern Uli Hoeness amesema hiyo haimaanishi chochote kwa wakati huu wa msimu. Ushirikiano ulikuwa imara sana leo, tulilinda lango letu kwa uangalifu mkubwa sana. Hauwezi kuwazuia Bayern kwa dakika 90 na zaidi ya hilo tulikuwa hatari sana sana katika ushambuliaji, tulicheza vizuri mashambulizi ya mpigona tukawa hatari. Bila shaka ushirikiano ulikuwa mzuri sana leo.

Dortmund ililala mbele ya AugsburgPicha: Alexander Hassenstein/Getty Images

Wapinzani wa karibu wa Bayern Borussia Dortmund walipoteza nafasi ya kuwawekea shinikizo baada ya kuzabwa 2 – 0 na Augsburg ambao kwa sasa wako nafasi ya pili kileleni na pointi sita sawa na Hoffenheim. Manuel Akanji ni beki wa BvB "Walicheza kwa kujilinda sana na tulikuwa na wakati mgumu kupata nafasi za kufunga. Hakukuwa na muendelezo mzuri katika ushambuliaji na tulipoteza mipira sana katika ulinzi. Hatukuwa wakakamavu vya kutosha. Tulipiga shuti nyingi na kuudhibiti mpira, lakini nafasi za wazi za kufunga zilikuwa labda moja au mbili tu.

Awali macho yote yalielekezwa kwa mechi kati ya timu mbili zilizopoteza mastaa wao Timo Werner na Patrick Schick kwa upande wa RB Leipzig na Kai Havertz na Kevin Volland kwa upande wa Bayer Leverkusen. Na baada ya kipenga cha mwisho kupulizwa, zikaridhika na sare ya 1 – 1. Peter Bosz ni kocha wa Leverkusen. "Nadhani sare hiyo ni sawa kama umeutazama mchezo mzima. Lakini timu zote zingeshinda. Nadhani ulikuwa mchezo wa kufurahisha sana kwa sababu kulikuwa na timu mbili zilizotaka kushambulia na kuonyesha mchezo mzuri. Nadhani ilipendeza kututizama leo.

afp, reuters, ap, dpa

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW