Bayern sasa jukumu lake ni kuifukuza BVB
17 Desemba 2018Tukihamia katika ligi sasa , tuanze na Bundesliga: Bayern Munich imeanza kucheza kandanda linaloleta tija katika jukumu lake jipya ambapo hivi sasa jukumu lake ni kuifukuza Borussia Dortmund viongozi wa Bundesliga kwa sasa lakini timu hiyo kutoka jimboni Bavaria imeanza kurejea tena katika ushindi wakati ikiingia katika mtihani wake mkubwa dhidi ya RB Leipzig hapo Jumatano.
Bayern inapishana na Dortmund kwa pointi 9 wakati ikiingia katika mchezo wa katikati ya wiki na mwanya huo unaweza kuongezeka hadi pointi 12 , hata kama itakuwa ni kwa muda , iwapo Dortmund inayosafiri kwenda mjini Dusseldorf kupambana na Fortuna Dusseldorf kesho Jumanne.
Dortmund imeshinda michezo 6 ya Bundesliga mfululizo na kujenga mwanya huo dhidi ya Bayern Munich inayoshikilia nafasi ya tatu pamoja na Borussia Moenchengladbach , ambao wako katika nafasi ya pili kutokana na tofauti ya mabao ya kufunga.
Lakini baada ya kipindi cha kuyumba , Bayern wameanza kupata tena mbinu za ushindi kwa kushinda mata tatu mfululizo katika ligi na kufikia kilele chake mwishoni mwa juma kwa ushindi wa mabao 4-0 dhidi ya Hannover 96, ushindi ambao kocha Niko Kovac ameuita ushindi huo kama „moja ya mchezo wao mzuri kabisa msimu huu."
Leipzig , ambayo iko pointi 2 tu nyuma ya Bayern ikiwa katika nafasi ya nne, itatoa changamoto kubwa kuliko ilivyokuwa kwa kikosi cha Hannover 96 kilichoko mkiani katika msimamo wa ligi ya Ujerumani Bundesliga, lakini hali ya kujiamini imeanza kurejea katika kikosi cha Bayern.
Gladbach kupunguza mwanya
Gladbach inaweza kupunguza mwanya dhidi ya Dortmund hadi pointi sita, iwapo hata kama ni kwa muda tu, kwa pambano la mapema kesho Jumanne , ambapo inapambana na Nuremberg nyumbani. Kocha Dieter Hecking alikiri kwamba kikosi chake cha Gladbach kilikuwa na bahati tu kupata pointi moja katika mchezo dhidi ya Hoffenheim siku ya Jumamosi, ambapo timu hizo zilitoka sare bila kufungana, na pia kuwapoteza wachezaji muhimu kama Raffael na Lars Stindl ambaye huenda asiwemo katika kikosi kitakachopambana na Nuremberg.
Dortmund hivi karibuni iliwadhibiti mahasimu wao wakubwa Schalke 04 na pia kuwatupa kando Werder Bremen ambayo inawania kushiriki katika vikombe vya Ulaya msimu ujao na kufanikiwa kupata taji ambalo si rasmi la „mabingwa wa mapukutiko" kabla ya michezo miwili ya kukamilisha mzunguko wa kwanza wa Bundesliga.
Lakini kwa ubingwa wake wa kwanza tangu mwaka 2012, kukiwa na uwezekano wa hilo, kikosi hicho cha kocha Lucien Favre kina shauku kutoteleza dhidi ya Dusseldorf ambayo inapambana kutoshuka daraja , kabla ya kuukamilisha mwaka 2018 kwa pambano kali nyumbani dhidi ya Gladbach siku ya Ijumaa.
Bado tuna michezo miwili muhimu kabla ya kwenda katika mapumziko ya majira ya baridi na tunataka kuendelea na ushindi hali tuliyoionesha hadi sasa hadi mwisho wa nusu ya kwnza ya msimu ," amesema mlinda mlango Roman Burki.
Tunafurahia hali hii, lakini tunafahamu pia kwamba hali inaweza kubadilika haraka.tunapaswa kufanya kila liwezekanalo katika uwezo wetu kubakia juu." Mapambano ya kesho Jumanne ni pamoja na Hertha Berlin ikiikaribisha Augsburg na Wolfsburg inaikaribisha VFB Stuttgart, ambayo huenda haitakuwa na nahodha wake Christian Gentner kutokana na kuomboleza kifo cha baba yake aliyefariki siku ya Jumamosi baada ya ushindi wa Stuttgart dhidi ya Hertha Berlin.
Mwandishi: Sekione Kitojo / rtre / afpe / ape
Mhariri: Iddi Ssessanga