Bayern waangazia macho DFB Pokal
15 Aprili 2013Bayern wanawaalika Wolfsburg katika nusu fainali ya kombe hilo. Katika fainali ya mwaka jana, Bayern waliduwazwa magoli matano kwa mawili na Borussia Dortmund. Lakini miamba hao ya soka Ujerumani, imejifunga kibwebwe msimu huu, na kuipokonya Dortmund taji la Bundesliga, ikiwa ndio timu ya kwanza kushinda taji la ligi mapema kabla ya msimu kukamilika.
Wakati lengo lao likisalia kuwa Champions League, kocha Jupp Heynckes hajalipuuza kombela Shirikisho ambalo alilishinda kama mchezaji wa klabu ya Borussia Moenchengladbach mnamo mwaka wa 1973.
Heynckes analenga kutwaa mataji matatu kabla ya kumkabidhi mikoba ya majukumu Pep Guardiola, ambaye atamrithi mwishoni mwa msimu huu. Hayo yanajiri wakati viongozi wa Bayern wakituliza matamshi yaliyotolewa na mshauri wa mshambuliaji Mario Gomez ambaye anasema mchezaji huyo wa timu ya taifa ya Ujerumani hafurahishwi na jukumu lake kwa sasa kama mchezaji wa akiba.
Mwenyekiti Karl Heinz Rummenige anasema kwa sasa hajui kile Gomez anakipanga, hivyo watasubiri ili kuona. Gomez hajaweza kujumuishwa katika kikosi cha kwanza msimu huu baada ya kurejea kutoka mkekani, lakini alifunga goli katika ushindi wao wa mabao manne kwa sifuri Jumamosi dhidi ya Nuremberg, wakati kocha akiwapumzisha wachezaji wake tisa wa kikosi cha kwanza ikiwa ni pamoja na Mario Mandzukic.
Hilo lilikuwa goli lake la nane kwa Gomez ambaye mkataba wake na Bayern unakamilika mwaka wa 2016. Sasa yeye na Claudio Pizzaro wanawania nafasi ya kucheza nusu fainali ya Champions League mkondo wa kwanza dhidi ya Barcelona, wakati Mandzukic akitumikia adhabu ya kadi za njano. Wolfsburg walitoka sare ya kufungana magoli mawili kwa mawili mwishoni mwa wiki. Katika mchuwano mwingine wa nusu fainali ya DFB Pokal, siku ya Jumatano, VfB Stuttgart wanawaalika Freiburg.
Bayern wana pointi 78 na wamebaki tu na pointi tatu wakifikia rekodi ya Dortmund ya mwaka jana ya pointi 81, zikiwa zimesalia mechi tano msimu kukamililka. Dortmund wako katika nafasi ya pili na pointi 58, baada ya kuwagwangura washika mkia Greuther Fürth mabao sita kwa moja, mchuwano ambao mkufunzi wa Real Madrid Jose Mourinho alikuwa mmoja wa mashabiki waliofika uwanjani kushabikia Dortmund…na bila shaka alikuwa na lengo moja tu…kuziangalia mbinu za mwenzake Jurgen Klopp kabla ya kupambana nao katiuka nusu fainali ya Champions League.
Bayer Leverkusen wako katika nafasi ya tatu na pointi 50, baada ya kutoka sare ya magoli mawili kwa mawili na nambari nne Schalke katika mpambano wa kusisimua. Schalke wana pointi 46. Katika mechi nyingine ya Bundesliga Augsburg, iliimarisha nafasi zake za kuepuka shoka la kushushwa daraja, baada ya kuishinda Eintracht FRANKFURT magoli mawili kwa sifuri jana Jumapili.
Mwandishi: Bruce Amani/AFP/DPA/Reuters
Mhariri: Mohammed Khelef