1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Bayern waangukia pua, Arsenal waishangaza Madrid

9 Aprili 2025

Matumaini ya Bayern Munich kushinda mataji mawili msimu huu yameingia doa baada ya kulazwa 2-1 na Intermilan nyumbani usiku wa kuamkia Jumatano katika mechi ya mkumbo wa kwanza ya robo fainali Ligi ya Mabingwa Ulaya.

Fußball Champions League | Bayern München - Inter Mailand
Harry Kane baada ya kukosa nafasi ya wazi ya kufunga dhidi ya Inter MilanPicha: Sven Hoppe/dpa/picture alliance

Haya yanafanyika wakati ambapo Arsenal wameushangaza ulimwengu kwa kumcharaza bingwa mtetezi Real Madrid magoli 3-0 katika uwanja wao wa nyumbani Emirates, huko mjini London katika mechi nyengine ya robo fainali.

Huko mjini Munich, Intermilan waliingia uongozini kunako kipindi cha kwanza kupitia mshambuliaji wao matata raia wa Argentina Lautaro Martinez, muda mfupi baada ya mshambuliaji wa Bayern Harry Kane kugonga mwamba na kukosa kuwaweka kifua mbele vinara hao wa Bundesliga.

Mchezaji wa akiba Thomas Müller ambaye alitangaza Jumamosi iliyopita kwamba ataihama Bayern mwishoni mwa msimu, alionekana kana kwamba ameiokoa Bayern kwa kufunga goli la kusawazisha dakika tano kabla medchi kufikia mwisho ila dakika tatu baadae, Davide Frattesi akawafungia Inter goli la ushindi.

Mshambuliaji wa Bayern Thomas Müller baada ya mechi na InterPicha: Sven Hoppe/dpa/picture alliance

Mara ya mwisho Bayern kufungwa nyumbani ilikuwa 2021

Kocha wa Bayern Vincent Kompany anasema ana matumaini kwamba nafasi bado wanayo kutinga nusu fainali.

"Tumepoteza 2-1 na siwezi kufanya lolote kulibadilisha hilo sasa. Ila si sahihi kusema kwamba matokeo haya ya 2-1 yanaonesha kwamba hatukuwa katika nafasi ya kuishinda mechi hii, sicho kilichotokea. Ila matokeo ni ya Inter, hongera kwao. Wiki ijayo bado tuna matumaini kamili kwamba tunaweza kuishinda mechi," alisema Kompany.

Matokeo hayo yalifikisha mwisho rekodi ya Bayern ya kutofungwa nyumbani katika mechi za ligi ya mabingwa ambapo mara ya mwisho kupoteza mechi hapo Allianz Arena ilikuwa Aprili 7 mwaka 2021 dhidi ya Paris Saint Germain.

Inter sasa wana matumaini ya kurudi katika uwanja huo huo wa Allianz Arena mnamo Mei 31 kucheza fainali, ila kwanza ni mpaka wapambane na Bayern tena katika mkumbo wa pili huko San Siro Jumatano ijayo ambapo mshindi atacheza na ama Barcelona au Borussia Dortmund.

Kwengineko usiku wa Jumanne huko London mikwaju miwili ya frikiki kutoka kwa Declan Rice na shuti kama la mshambuliaji la Mikel Merino yalitosha kuwaangamiza mabingwa watetezi Real Madrid mikononi mwa Arsenal walipolemazwa 3-0.

Arsenal walionekana kuutawala mchezo katika vipindi vyote ila kipindi cha kwanza kiliishia sare ya kutofungana na katika kipindi cha pili ndipo walipowalemea hao wapinzani wao wa Uhispania.

Kiungo wa Arsenal Declan Rice baada ya kufunga goli la kwanza dhidi ya Real MadridPicha: Izzy Poles/News Images/Avalon/Photoshot/picture alliance

Real watajaribu kukipindua kipigo hicho cha Arsenal Jumatano ijayo uwanjani Santiago Bernabeu huko Madrid Uhispania ila wamepata pigo kwa kuwa kiungo wao mkabaji Eduardo Camavinga hatoshiriki mechi hiyo baada ya kuonyeshwa kadi nyekundu Jumanne.

"Usiku kama huu mambo ni mawili tu, moja ni mazingira tuliyoweka robo saa kabla mechi, kitu ambacho sijawahi kukiona. Kwa hiyo kucheza na nguvu ile, na dhamira ile na mashabiki wetu ni mambo yaliyoleta tofauti kubwa. Kisha umahiri wa mchezaji binafsi ulioamua mechi na mabao mawili ya kwanza ya Declan Rice, nafikiri yanaeleza usiku ulivyokuwa," alisema Arteta.

Madrid kwa sasa wamekubali mabao 11 langoni mwao katika mechi zao 4 zilizopita kwenye mashindano yote huku historia ikionyesha kuwa Arsenal hawajapoteza mechi ya ligi ya mabingwa wakiwa wako kifua mbele kwa magoli matatu kwenye duru ya kwanza.

Wafungaji wawili bora wa Ligi ya Mabingwa kupatana

Mshindi wa robo fainali hii atapambana na ama Aston Villa au PSG katika nusu fainali.

Na usiku wa Jumatano mechi mbili nyengine za robo fainali zitachezwa Barcelona wakiwa wenyeji wa Borussia Dortmund ya Ujerumani na Aston Villa wawatembelee Paris Saint Germain huko Ufaransa.

Katika mechi ya Dortmund na Barca, wafungaji wawili bora katika mashindano ya ligi ya mabingwa msimu huu watapatana, Robert Lewandowski wa Barcelona aliye na mabao 11 kufikia sasa na Serhou Guirassy raia wa Guinea anayeichezea Dortmund akiwa na mabao 10.

Wote wawili walifunga Barcelona waliposhinda 3-2 katika mechi ya makundi huko Dortmund. Dortmund lakini watakuwa bila beki wao wa kati Nico Schlotterbeck ambaye atakuwa nje kwa miezi sita kutokana na jeraha la goti.

Katika hiyo mechi nyengine Paris Saint Germain ambao wanatafuta taji lao la kwanza la ligi ya mabingwa watakuwa wakicheza na Aston Villa, timu nyengine ya England, baada ya kuiondoa Liverpool kwenye hatua ya kumi na sita bora.

Vyanzo: DPA/AP

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW