Bayern wamebeba taji la tisa mfululizo la Bundesliga
10 Mei 2021Ni baada ya mchezo wa kusisimua kati ya nambari mbili RB Leipzig na Borussia Dortmund iliyohitaji pointi tatu ili kurejea katika nafas iza nne bora. Na baada ya BVB kuwafunga Leipzig 3 – 2, ikamaanisha kuwa Bayern sasa wangetoa mvinyo na kusherehekea ubingwa wao wa tisa mfululizo wa Bundesliga.
Na waliingia uwanjani na kuwabamiza Borussia Moenchengladbach 6 – 0 huku mshambuliaji Robert Lewandowski akifunga hattrick na kufikisha mabao 39. Amebakisha bao moja tu akiifikia rekodi iliyowekwa na Gerd Mueller ya kufunga mabao 40 ya BUNDESLIGA katika msimu mmoja.
Kinyang'anyiro cha kucheza ligi ya mabingwa ya Ulaya kimepamba moto baada ya Eintracht Frankfurt kulazimishwa sare ya 1 – 1 na Mainz na kupoteza nafasi ya kuichukua tena nafasi ya nne kutoka kwa Dortmund. Mainz wako katika nafasi ya 12 na wanaonekana kuwa salama katika vita vya kushuka daraja. Sare hiyo ya Frankfurt pia ina maana kuwa Leipzig imejihakikishia kandanda la Ligi ya Mabingwa msimu ujao.
Nambari mbili kutoka mkiani Cologne ipo katika eneo baya la kushushwa ngazi moja kwa moja huku zikiwa zimesalia mechi mbili tu. Ni baada ya kufungwa 4 – 1 na Freiburg. Lakini washika mkia wenzao Arminia Bielefeld walitoka sare tasa na Hertha Berlin. Wao pamoja na Werder Bremen, wako juu ya GOLONE na pengo la pointi mbili. Hertha na mechi moja mkononi. Schalke wameshaiaga Bundesliga kwa hivyo vita vya kuepuka kushuka daraja vitaamuliwa siku ya mwisho.
AFP/AP/Reuters