Vijana wa Pep walicheza mechi tatu za kirafiki China
24 Julai 2015Arturo Vidal, ambaye siyo mgeni katika kandanda la Ligi Kuu ya Ujerumani – Bundesliga maana aliwahi kuichezea Bayer Leverkusen kwa misimu minne hadi mwaka wa 2011, ameshinda mataji manne mfululizo ya ligi ya Italia Serie A na kuisaidia Juve kufika katika fainali ya Kombe la Mabingwa msimu uliopita, ambapo walishindwa na Barcelona.
Vidal mwenye umri wa miaka 28 pia aliisaidia Chile kushinda Kombe la Mataifa ya Amerika Kusini – Copa America kwa mara ya kwanza katika ardhi ya nyumbani mapema mwezi huu, na anatarajiwa kujiunga na wenzake wa timu ya Bayern mapema wiki ijayo, kwa mujibu wa kiongozi wa Bayern Karl-Heinz Rummenige
Dortmund: msimu mpya, malengo mapya
Borussia Dortmund ilimaliza enzi ya kocha Juergen Klopp kwa matokeo ambayo hayakuridhisha lakini sasa afisa mkuu mtendaji Hans-Joachim Watzke ana matumaini kuwa kocha mpya Thomas Tuchel atafanikiwa kuyabadilisha matokeo hayo katika kipindi kifupi.
Watzke anasema BVB wanataka kurudi katika kikundi cha timu nne bora za Bundesliga na pia kurejea katika Champions League. Amesema “yeyote ambaye ana majina kama (Mats) Hummels, (Ilkay) Guendogan,
(Marco) Reus na (Pierre-Emerick) Aubameyang hawezi kuwa katika nafasi mbaya kama yetu”
Kiongozi huyo anaamini kuwa kikosi cha Dortmund ni imara na chenye uwezo wa kushindana na timu zilizomaliza katika nafasi nne za kwanza msimu uliopita. Bayern ilishinda taji la Bundesliga na pengo kubwa huku Wolfsburg, Borussia Moenchengladbach na Bayer Leverkusen zikifuata nyuma. BVB ilimaliza nyuma ya Leverkusen na pengo la pointi 15.
Mwandishi: Bruce Amani/AFP/DPA/AP
Mhariri: Iddi Sessanga