Bayern washerehekea taji la nane la Bundesliga
17 Juni 2020Sherehe za mwaka huu hata hivyo ni tofauti kabisa na miaka saba iliyopita. Wachezaji walishangilia na kupiga kelele katika uwanja ambao haukuwa na mashabiki baada ya kuishinda Werder Bremen 1-0 siku ya Jumanne (16.06.2020)
Vyombo vya habari vimeitaja timu ya Bayern kama "Geister-Meister" yaani washindi bandia. "Kushangilia bila mashabiki ni ngumu kidogo," Lewandowski aliimbia televisheni ya Sky. "Mandhari yanakosekana na kitu kingine, sio ari, bali upendo wa mashabiki," aliongeza kusema mshambuliaji huyo hatari wa Bayern Munich, raia wa Poland.
Mechi hiyo ambayo ilihakikisha ushindi wa taji la Bundesliga haukuwa wa kawaida kwa Bayern ambayo imekuwa na tabia ya kufunga idadi kubwa ya magoli. Bao la Robert Lewandowski liliisaidia Bayern kupata ushindi wa tabu dhidi ya Werder Bremen. Mechi hiyo iliyochezea uwanja wa Weserstadion mjini Bremen iligeuka kuwa vita kali baada ya beki wa kushoto wa Bayern Munich, Alphonso Davies, kuonyeshwa kadi nyekundu na kutolewa nje ya uwanja dakika ya 79.
Kama si hatua ya dakika za lala salama ya kipa Manuel Neuer kuokoa bao la wazi la Bremen kwa mkono mmoja, shamra shamra za kushangilai ushindi wa taji la nane mfululizo zingesuburi kwanza.
Ushindi wa Bayern unaiweka alama kumi mbele ya timu inayoshikilia nafasi ya pili katiak msimamo wa ligi, Borussia Dortmund, ambayo inaweza kupata alama tisa kutoka kwa mechi tatu zilizosalia kabla msimu kukamilika.
(ap)