1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Bayern yaanza msimu mpya kwa ushindi

25 Agosti 2018

Msimu mpya wa ligi kuu ya kandanda hapa Ujerumani - Bundesliga umeanza rasmi ambapo mabingwa Bayern Munich walifunga mabao mawili katika dakika nane za mwisho na kuwazaba wageni wao Hoffenheim mabao matatu kwa moja.

Fußball Bundesliga FC Bayern München - TSG 1899 Hoffenheim
Picha: Reuters/M. Dalder

Mshambuliaji wa Bayern Robert Lewandowski alifunga penalti yenye utata katika dakika ya 82, wakati Arjen Robben akifunga la tatu katika dakika ya 90 baada ya kasi ya Hoffenheim kupungua.

Thomas Mueller aliwaweka kifua mbele mabingwa hao chini ya kocha mpya Nico Kovac alipofunga bao la kichwa katika dakika ya 23, lakini Adam Szalai alisawazisha katika dakika ya 57.

Ushindi huo ulikuja hata hivyo ulikuja na habari mbaya kwa Bayern, ambao wameshinda mataji sita ya Bundesliga mfululizo, baada ya kiungo Kingsley Coman kuondolewa uwanjani kutokana na tatizo la kifundo cha mguu. Ulikuwa ni mchuano wake wa kwanza wa ligi tangu alipomua msuli mwezi Februari.

Penalti ya Bayern ilizusha utataPicha: picture-alliance/dpa/S. Hoppe

Akizungumza baada ya mechi hiyo, kocha Kovac alisema kuwa walistahili ushindi huo lakini ni wazi kuwa haukupatikana kwa urahisi kama ilivyoonekana baada ya mechi. Mlinda mlango Manuel Neuer alicheza mechi yake ya kwanza ya ligi katika miezi 11.

Mchuano huo hata hivyo ulikumbwa na utata wakati Bayern walipewa penalti baada ya Frank Ribery kuchezewa visivyo. Picha zilimuonyesha Ribery akijiangusha kwenye kijisanduku akiidai kuwa alipigwa kiatu na beki wa Hoffenheim Havard Nordtveit.

Kocha wa Bayern alikiri kuwa hawakustahili kupata penalti hiyo. "Nisingepeana penalti hiyo," alisema Kovac , wakati mwenzake wa Hoffenheim, Julian Nagelsmann akionekana kushikwa na hamaki. Nagelsmann aliwashooshea kidole cha lawama waamuzi wanaosaidia kwa kuangalia video.

Mwandishi: Bruce Amani/AFP/Reuters
Mhariri: Jacob Safari

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW