1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Bayern yatanua mwanya wa pointi 9 kileleni

19 Desemba 2021

Borussia Dortmund iliangukia kipigo kwa mara tano kwenye ligi msimu huu, baada ya kucharazwa 3-2 na wenyeji wao Hertha Berlin na kuiwezesha Bayern Munich kufungua mwanya wa pointi tisa kileleni mwa Bundesliga.

Bundesliga | Hertha BSC- Borussia Dortmund
Picha: Andreas Gora/picture alliance

Julian Brandt aliipatia Dortmund bao la kuongoza katika kipindi cha kwanza, lakini Hertha Berlin ilirudi kwa kishindo. Ishak Belfodi aliisawazishia na kisha Marco Richter akacheka na wavu mara mbili.

Haaland hakuwa na mkwaju hata mmoja kwenye goli na alionyesha kufadhaika kwake huku Hertha ikipigana vikali kutoka filimbi ya kwanza ya mchezo.

Bayern yaendelea kutamba

Picha: Christof Stache/AFP/Getty Images

Siku ya Ijumaa Bayern waliwazaba Wolfsburg mabao 4-0 na wataanza mwaka mpya kama wachezaji wanaopewa nafasi kubwa ya kushinda taji la Bundesliga mara 10 mfululizo.

Hapo awali, Eintracht Frankfurt waliendelea kupanda jedwali kwa ushindi wa sita katika michezo saba huku fowadi wa Denmark Jesper Lindstrom akifunga kwa mechi ya tatu mfululizo na kupelekea ushindi wa 1-0 dhidi ya Mainz.

Union Berlin ilishika nafasi ya sita sawa na Frankfurt kwa pointi 27 pongezi kwa mshambuliaji wa zamani wa Ujerumani Max Kruse, ambaye alifunga bao pekee katika ushindi wa 1-0 dhidi ya Bochum siku mbili baada ya kufunga ndoa.

Hoffenheim inayoshika nafasi ya nne iliambulia sare ya 1-1 nyumbani na Borussia Moenchengladbach baada ya beki Kevin Akpoguma kufunga bao la dakika za mwisho.

Gladbach, ambao walikuwa wamepoteza michezo yao minne ya awali ya ligi, walichukua uongozi wa kipindi cha kwanza kupitia mshambuliaji wa Breel Embolo.

Tadesco apata kipigo cha kwanza

Picha: Thomas Eisenhut/Getty Images

Domenico Tedesco alipata kipigo chake cha kwanza katika mechi tatu akiwa kocha wa RB Leipzig, ambao walipoteza 2-0 nyumbani kwa wachezaji 10, Arminia Bielefeld.

Fabian Klos aliyetokea benchi wa Bielefeld alionyeshwa kadi nyekundu kwa kumchezea vibaya beki wa Leipzig Willi Orban mara baada ya kuingia uwanjani.

Licha ya kutolewa kwa mchezaji wao, Bielefeld ilipata ushindi huo wakati kiungo wa kati wa Japan Masaya Okugawa alipofunga bao zikiwa zimesalia dakika 15.

Greuther Fuerth sasa wako nyuma kwa pointi 11 mkiani mwa jedwali baada ya sare tasa nyumbani dhidi ya Augsburg.

Arsenal katika nafasi ya 4 bora

Huku haya yakijiri Arsenal ilijiimaarisha kwa kuifunga Leeds 4-1 katika mechi ya pekee ya Ligi Kuu jana Jumamosi wakati wimbi jipya la Corona likisabisha mechi kadhaa kuahirishwa.

Picha: Andre Boyers/AP/picture alliance

Ni mechi nne pekee ambazo sasa zinastahili kuchezwa katika jumla ya mechi 10 ambazo zilitarajiwa kuchezwa wikendi hii, huku janga hilo likizidi kusababisha machafuko wakati wa shughuli nyingi zaidi katika kalenda ya soka ya Uingereza.

Mechi tatu bado zimeorodheshwa Jumapili pambano la Manchester City na Newcastle, Wolves na Chelsea na Tottenham na Liverpool.

Mkutano wa vilabu vya Ligi ya Premia siku ya Jumatatu unatazamiwa kuamua iwapo wataendelea na nia ya kucheza michezo mahali ambapo ni salama au kusimamisha kwa muda kampeni hiyo kama njia ya kuzuia maambukizi.

 

/AFP