Bayern yainyoa Borussia Dortmund
5 Oktoba 2015Mbio za kuwania ubingwa wa ligi ya Ujerumani Bundesliga , zimevurugika, kama vile mtu ametumbukiza msumari mrefu katika tairi ya gari.
Kipigo cha mabao 5-1 , mabingwa watetezi na viongozi wa ligi ya msimu huu Bayern Munich ilichotoa dhidi ya Borussia Dortmund ambayo iko katika nafasi ya pili katika msimamo wa ligi , kinaeleza wazi kwamba Bayern ni mshindi asiyeshindika na licha ya kwamba si vizuri kusema bingwa amekwisha amuliwa wakati tuko katika mwezi wa Oktoba, lakini dalili zote zinaonesha mwelekeo huo.
Kwa heshima ya vilabu vingine vinavyoshiriki Bundesliga, si vizuri kuitawaza Bayern Munich ubingwa katika wakati huu, lakini kwa ushindi wa nane mfululizo, na jinsi walivyoshinda jana Jumapili inaonesha kwamba shauku ya mvutano kwa ubingwa katika Bundesliga imefutika tena mapema mno mwanzoni mwa msimu.
Si ajabu kwamba kikosi cha Pep Guardiola kimeshinda mchezo huo dhidi ya BVB lakini jinsi kilivyoshinda , na jinsi gani timu hiyo mabingwa wa Ujerumani ilivyoweza kuishinda timu inayoishika nafasi ya pili katika msimamo wa ligi.
Timu iliyoko katika nafasi ya juu ya msimamo wa ligi haikustahili kufungwa kama ilivyotoa zawadi bao la kwanza na la tatu, kwa Bayern , wanaeleza wadadisi wengi wa michezo nchini Ujerumani. Mipira ya mbali mita 40 aliyoitoa mlinzi wa Bayern Jerome Boateng na kupachikwa wavuni kwanza na Thomas Mueller na kisha Robert Lewandowski yameiweka wazi safu ya ulinzi ya Borussia Dortmund na kumkanganya mlinda mlango Roman Burki.
Jerome Boateng anasema:
"Tulicheza vizuri sana. Baada ya dakika 15 tulikuwa katika hali ya uchangamfu kabisa na kisha tukaanza kupata kile tulichokitaka. Hata kwa kiwango cha magoli, tumestahili kushinda na bila ubishi, tumeonesha kwamba tuko mbali."
Lazima tukubali , kwamba , washambuliaji Muller na Lewandowski ni vifaa vya kufumania nyavu vyenye ufundi wa hali wa juu kabisa. Lakini kuwarahisishia namna ilivyokuwa haipaswi kabisa kutokea. kama anavyoeleza mchezaji wa kati wa Borussia Dortmund Ilkay Gundogan.
"Makosa yale yale mara mbili katika kipindi cha kwanza, na kufungwa mabao yale, kwa mpira wa mbali ambao umepita walinzi wetu. Kuhusiana na penalti dhidi yetu, tulikuwa tumeupeleka mpira kwa aadui halafu ukarejea kwetu haraka. Huu ni upuuzi, hii huenda pia ni kwa kiasi fulani kutokuwa makini vya kutosha."
Timu zinazoifuata Bayern
Borussia Dortmund iliingia katika mchezo wa jana Jumapili ikiwa ni timu ya pili ambayo haijapoteza mchezo msimu huu baada ya Bayern . Wengi walikuwa na ndoto , kwamba BVB baada ya kumpata kocha Thomas Tuchel , akichukua nafasi ya kocha maarufu Jurgen Klopp , kwa usiku mmoja tu inaweza kurejea katika kiwango chake na kuwa tena mpinzani wa Bayern.
Mchezo wa jana umeonesha wazi kwamba bado kuna masafa marefu kwa BVB kuweza kuwafikia tena Bayern.
Na wawindaji wengine wa Bayern ,kama makamu bingwa VLF Wolfsburg wameuza sehemu ya nguvu yao Kevin de Bruyne kwa Manchester City. Borussia Moenchengladbach inaonesha kupanda kidogo kiwango kwa sasa, lakini na yenyewe ni mgonjwa anayehitaji matibabu, na inawaambukiza wengine ugonjwa.
FC Schalke 04 imeangukia pua jana Jumapili pia kwa kuraruliwa kwa mabao 3-0 na FC Kolon. Na Bayer Leverkusen inapambana kwa kiasi kikubwa dhidi yake binafsi badala ya wengine. Ilitoka sare jana ya bao 1-1 dhidi ya Augsburg , baada ya mlinda mpango Bern Leno kujifunga mwenyewe.
"Nafikiri kutokana na jinsi tulivyocheza hapa ni lazima tujilaumu. Kwasababu iwapo nisingefungwa bao la kijinga namna ile, huenda mchezo ungekuwa vingine kabisa. Na tulipopata mkwaju wa penalti pia mambo hayakuwa mazuri. Nafikiri, ilikuwa siku mbaya kwetu."
Katika Bundesliga kwa sasa hakuna timu inayoweza kupimana nguvu sawa na Bayern Munich . Shauku ya kupata mvutano katika Bundesliga ; tusahau.
Premier League
Katika ligi ya Uingereza Premier League , sare ya bao 1-1 iliyopata Liverpool dhidi ya mahasimu wao wakubwa Everton jana haikutosha kumuokoa kocha Brendan Rodgers kutupiwa virago vyake nje. Baada ya saa chache Rodgers kusema kwamba "anamatumaini ya kuendelea kuwapo katika timu hiyo, klabu hiyo ilitangaza kuachana nae.
Liverpool sasa imeanza kumtafuta mrithi wa kiti cha Brendan Rodgers, lakini yeyote atakayekuja atakabiliana na masuala kadhaa yaliyosababisha matatizo katika kilabu hicho.
Liverpool itahitaji kocha anayeona mbali kwa darubini kali, kocha atakayekuwa tayari kuchafua mikono yake katika kujenga na kuwaendeleza wachezaji, badala ya kocha ambaye atabadilisha mambo haraka.
Inaonekana kwa mtazamo huo anayeweza kuifanya kazi hiyo ni kocha mwenye sifa nyingi Mjerumani aliyekuwa akiiongoza Borussia Dortmund Jurgen Klopp.
Kocha wa Ajax Amsterdam Frank de Boer huenda akafikiriwa, lakini inaweza kuwa pia kocha wa zamani wa Chelsea na Real Madrid Carlo Ancelotti.
Kampuni inayomiliki klabu ya Liverpool Fenway Sports Group, FSG italazimika kufanya uamuzi wa busara sana katika hatua hii , ili kuweza kupata kuungwa mkono na mashabiki wa Liverpool, kwa kuwa mpasuko unaonekana wazi.
Sergio Aguero alipachika mabao matano wakati Manchester City waliopoichana chana Newcastle United kwa mabao 6-1 na majirani zao Manchester United waliogelea katika kipigo cha mabao 3-0 dhidi ya Arsenal London, ambapo kocha wa kikosi hicho cha mjini London Arsene Wenger amesema ushindi wa jana dhidi ya Manchester United unatoa jibu kwa baadhi ya wakosoaji wake.
Wenger amekosolewa sana katika vyombo vya habari vya Uingereza baada ya kikosi chake kushindwa na Olympiakos Pireus wiki iliyopita katika mchezo wa Champions League wakati timu hiyo ikiwa na wakati mgumu na kukaribia kuyaaga mashindano hayo katika awamu ya makundi kwa kumpanga mlinda mlango mwenye makosa mengi David Ospina.
Barcelona chali, Real yavutwa shati
Katika La Liga , nchini Uhispania Atletico Madrid ilipata bao la mchezaji wa akiba Luciano Vietto na kupata sare ya bao 1-1 dhidi ya Real Madrid jana Jumapili.
Viongozi wa ligi hiyo Villareal walipoteza mchezo wao dhidi ya Levante kwa bao 1-0 na Barcelona ilipoteza mchezo wao kwa kupachikwa mabao 2-1 dhidi ya Sevilla siku ya Jumamosi.
Na katika Serie A , nchini Italia, AC Milan ilikubali kipigo cha mabao 4-0 dhidi ya SSC Napoli jana Jumapili. Fiorentina inaendelea kushikilia nafasi ya kwanza katika msimamo wa ligi baada ya kuishinda Atalanta nyumbani kwa mabao 3-0.
Kombe la shirikisho CAF
Katika bara la Afrika ule mpambano wa fainali baina ya mahasimu wa Misri Al-Ahly na Zamalek umeepukwa katika kombe la shirikisho CAF, baada ya Orlando Pirates ya Afrika kusini kufanikiwa kuingia fainali kwa kuiangusha Al-Ahly ya Misri jana Jumapili.
Orlando Pirates itaingia katika fainali dhidi ya Etoile Sahil ya Tunisia katika fainali itakayochezwa nyumbani na ugenini.
Orlando ilifanikiwa kuiangusha Al-Ahly kwa jumla ya mabao 5-3, na fainali itafanyika Novemba 20 na 29 mchezo wa kwanza ukifanyika Afrika kusini.
Kufungwa kwa Al-Ahly, washindi wa mataji 29 ya shirikisho la kandanda barani Afrika CAF, kumekamilisha wiki ya maafa kwa vilabu vya Misri wakati majirani zao Zamalek pia walikubali kipigo cha jumla ya mabao 5-3 licha ya kushinda mchezo wa mwisho kwa mabao 3-0 mjini Cairo, lakini katika mchezo wa kwanza ilikubali kipigo cha mabao 5-1 dhidi ya Etoile.
Mtoto wa Blatter amtetea baba yake
Wivu na chuki miongoni mwa vyombo vya habari ndio kilichoiharibu sifa ya rais wa shirikisho la kandanda duniani FIFA Sepp Blatter, amesema mtoto wa kike wa kiongozi huyo jana katika mahojiano yaliyochapishwa katika gazeti la Uswisi la Blick.
"Vyombo vya habari vimechafua heshima yake. Kwanini wanamtafuta sana? Kitu gani amewafanyia? sifahamu," amesema Corinne Blatter, ambaye alikuwa mshauri wake mkuu wakati akipanda ngazi za uongozi katika shirikisho hilo la kandanda duniani.
Blatter amekumbwa na kashfa kubwa katika FIFA mwezi uliopita wakati waendesha mashitaka wa Uswisi walipofungua uchunguzi wa kihalifu dhidi yake kuhusiana na matumizi mabaya ya fedha.
Siku ya Ijumaa wadhamini wakuu wa FIFA kutoka Marekani, Coca Cola, Visa, McDonald na Budweiser walimtaka Blatter ajizulu mara moja, wakisema kubaki kwake katika shirikisho hilo kunakwaza mabadiliko yanayohitajika.
Uchunguzi wa Doping
Uchunguzi wa matumizi ya madawa ya kuongeza nguvu misuli , doping utafanyika kwa haraka na huru zaidi hapo baadaye kuhakikisha wachezaji ambao wako safi hawachafuliwi sifa zao kwa uvumi wa kupatikana na makosa hayo, amesema rais wa chama cha riadha duniani IAAF Sebastian Coe leo.
Coe amerudia nia yake ya kurejesha hali ya kuaminika baada ya shirikisho la kimataifa la vyama vya riadha kujikuta imegubikwa na madai ya doping wakati wa kuelekea katika michezo ya riadha ya dunia mwezi Agosti, ambapo Kenya ilinyakua nafasi ya kwanza kwa wingi wa medali.
Na wakati akizungumza na wachezaji wa kikosi cha Kenya baada ya kupata ushindi huo mwishoni mwa juma , rais wa Kenya Uhuru Kenyatta amesema nchi hiyo itapambana na tatizo hilo.
"Tuna changamoto nyingi kwasababu wako wale ambao wanajaribu kuvuruga ushindi wetu kwa doping. Nafikiri tunapaswa kufanyakazi kwa pamoja kama familia kuhakikisha tunapambana na suala hilo. Kwasababu nafahamu hatuko hivyo. Tunashinda kwasababu ya vipaji vyetu. Mnashinda kwa kuwa mnavipaji. Hilo ndio linalotufanya tushinde."
Pistorius kujadiliwa
Na nchini Afrika kusini, bodi ya msahama inatarajiwa kuketi leo Jumatatu kuamua iwapo mwanariadha anayekimbia kwa miguu ya bandia Oscar Pistorius anapaswa kuachiwa huru kutoka gerezani kwa kumuua mpenzi wake.
Pistorius mwenye umri wa miaka 28 alihukumiwa mwaka jana kwenda jela miaka mitano kwa kumuua mpenzi wake Reeva Steenkamp katika siku ya wapendanao mwaka 2013, wakati wa kesi yake ambayo ilivuta hisia duniani.
Alipatikana na hatia ya kuuwa kwa uzembe, sawa na kuuwa bila ya kukusudia, baada ya kusema wakati wa kesi hiyo kwamba alimpiga risasi mpenzi wake akiwa chooni kwasababu alidhani kuwa ni mtu aliyeingia katika nyumba hiyo kwa nia ya wizi ama kutaka kuwadhuru yeye na mpenzi wake.
Mwandishi: Sekione Kitojo / afpe / dpae / rtre
Mhariri: Josephat Charo