1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Bayern yainyoosha BVB

Sekione Kitojo
8 Aprili 2019

El Klassiker, pambano linalokutanisha timu mbili vigogo nchini Ujerumani Bayern Munich na Borussia  Dortmund, limefanyika, lakini  haikuwa El Klassiker halisi. Borussia  Dortmund ilikubali kipigo cha mabao 5-0.

Bundesliga Bayern München gegen Borussia Dortmund
Picha: Reuters/K. Paffenbach

Ule mchezo  ambao  ulikuwa  ukisubiriwa kwa  hamu  kubwa  kati  ya  Bayern Munich na  Borussia  Dortmund hatimaye  ulifanyika  siku  ya  Jumamosi, lakini  pambano  hilo linalofahamika  kama  Klassiker  hapa  Ujerumani  halikukidhi matarajio  ya  wengi, pale  Borussia  Dortmund  iliposhindwa  kabisa kuhimili  vishindo  vya  kaka  mkubwa  Bayern Munich  na  kubugia mabao 5-0.

Wachezaji wa Borussia Dortmund wakiwa vichwa chini baada ya kupata kisago cha mabao 5-0 dhidi ya Bayern MunichPicha: picture-alliance/AP Photo/K. Joensson

Mchezo  huo ulikuwa ukisubiriwa kwa  shauku  kubwa kutokana  na  kwamba  mchezo  wa  kwanza  uliofanyika  katika uwanja  wa  Signal Iduna Park  mjini  Dortmund uliishia  kwa  ushindi wa  Dortmund  wa  mabao 3-2 dhidi  ya  Bayern Munich. Pili ni kwamba  Borussia  Dortmund  ilipoingia  katika  mchezo  huo  wa jumamosi  ilikuwa  ikiongoza jedwali  la  msimamo  wa  ligi  kwa pointi  mbili, mbele  ya  bayern Munich. 

Kwa  hivyo kila  mpenda kandanda  alitarajia  kwamba  mara  hii  ubingwa  wa  Ujerumani utaamuliwa  kwa  timu  hizo kuvutana. Lakini  yaliyotokea yanafurahisha:Bayern Munich iliirarua  bila huruma Borussia  Dortmund kwa  mabao 5-0 na kuwaburuza Dortmund muda wote jioni hiyo.

Serge Gnabry (kushoto)akipachika bao la nne la Bayern MunichPicha: Reuters/K. Pfaffenbach

Bayern Munich  kwa  ushindi  huo unaongoza  ligi  kwa tofauti  ya pointi moja , ikiwa  na  pointi 64  na  Borussia  Dortmund  ikiwa  na pointi 63. RB Leipzig imejiimarisha  katika  nafasi  ya  tatu ya msimamo wa  ligi kwa  kuwa  na  pointi 55, wakati Eintracht Frankfurt inakumbukia  enzi  zake  za  kina  JJ Okocha  na Antony Yeboah wakati  nayo  ikijiimarisha  katika  nafasi  ya  nne  ya  kucheza katika  Champions League msimu  ujao ikiwa  na  pointi 52. Frankfurt iliishinda  Schalke 04  siku  ya  Jumamosi  kwa  mabao 2-1, nyumbani  kwa  Schalke.

Mshambuliaji wa Schalke 04 akiwa amejiinamia baada ya kushindwa kufurukuta dhidi ya Eintracht FrankfurtPicha: Reuters/L. Kuegeler

Wakati  huo  huo upangaji  wa  timu zitakazopambana  katika  nusu fainali  ya  kombe  la  shirikisho  nchini Ujerumani , DFB Pokal ni kwamba  Bayern Munich  itakwaana  na  Werder  Bremen , na Hamburg SV itaikaribisha  RB Leipzig kuamua  nani  anakwenda Berlin  katika  fainali  ya  kinyang'anyiro hicho.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW