Bayern yakaribia taji la nne mfululizo
11 Aprili 2016Bayern Munich imesogea karibu na ubingwa wake wa nne mfululizo katika Bundesliga baada ya ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya VFB Stuttgart siku ya Jumamosi na kufungua mwanya wa pointi saba wakati ikibakia michezo mitano hadi mwisho wa ligi.
Borussia Dortmund inayoshikilia nafasi ya pili katika msimamo wa ligi, iliridhika na sare ya mabao 2-2 dhidi ya watani wa jadi Schalke 04 jana Jumapili wakati Hertha BSC Berlin , iliyoko katika nafasi ya tatu ilitoshana nguvu na Hannover iliyoko mkiani mwa ligi kwa mabao 2-2.
Nikitakiwa kuchagua kati ya ushindi wa mchezo wa watani wa jadi Derby na kufikia nusu fainali ya kombe la Uropa ligi , nitapenda kusonga mbele katika Europa League, amesema kocha wa BVB Thomas Tuchel katika mahojiano na kituo cha Sky kabla ya mchezo huo wa watani wa jadi.
BVB yawaweka nje wachezaji wake wa kikosi cha kwanza
Wachezaji wa kikosi cha kwanza wanane waliachwa nje na kocha huyo wa BVB katika mchezo huo muhimu wa watani wa jadi , siku nne kabla ya mchezo mwingine muhimu wa marudiano na FC Liverpool katika Europa League. Nisingependa kuhatarisha wachezaji wangu kuumia kutokana na hali ya michezo mingi muhimu msimu huu, amesema kocha Thomas Tuchel.
Katika mchezo wa jana ambao ulikuwa na kila hali ya ushindani na purukushani za uwanjani Tuchel ametoa tathmini ya katikati.
"Naridhika na jinsi tulivyocheza, lakini sijaridhika na mabao mawili tuliyofungwa. Baada ya bao la kusawazisha 2-2 tulipata nafasi nyingi za kuweza kupata mabao na katika kipindi cha kwanza pia tulipata nafasi nyingi, za kupata bao la kuongoza. Ndio sababu nahisi kulikuwa na uwezekano wa kupata ushindi. Lakini kwa hakika, kwa sare ya bao 2-2 hapa siwezi kulalamika."
Jana lilikuwapo pia pambano lingine la watani wa jadi kati ya FC Koln na Leverkusen. Leverkusen iliibuka jioni ya jana kidedea baada ya kuishinda FC Koln kwa mabao 2-0. Hata hivyo mchezo huo ulikuwa na hamasa tele na ukamalizika kwa timu zote kuwa na wachezaji 10 uwanjani baada ya mlinzi wa kushoto Wendel wa Leverkusen na Beaterncuop wa FC Kolon kutolewa nje kwa kadi nyekundu. Huyu hapa mlinda mlango wa Leverkusen Bernd Leno.
"Nadhani kila mtu amehisi kwamba hamasa ilikuwa kwa kiasi fulani juu mno, hata katika baadhi ya mapambano uwanjani. Tulitambua , kwamba tulipaswa kujiweka vizuri uwanjani, kwasababu wapinzani wameangukia pua. Ndio sababu ulikuwa ushindi muhimu sana. Lakini tunatambua pia, kwamba hatukucheza vizuri sana. Mara kadhaa tulitetereka na haukuwa mchezo sahihi kwetu. Lakini naamini kwamba muhimu ni kuwa tumeshinda, na kutia kibindoni pointi na muhimu zaidi hatukufungwa bao. Hii inatupa hali ya kujiamini zaidi kwa ajili ya michezo mitano ijayo."
Homa ya kushuka daraja yapanda Bundesliga
Homa ya kushuka daraja inazikumba timu karibu saba katika Bundesliga. TSG Hoffenheim ambayo mwezi mmoja uliopita ilikuwa katika nafasi ya moja kwa moja kushuka daraja imebadilisha majaaliwa yake na inamatumaini ya kubakia katika daraja la juu iwapo itafanya vizuri katika michezo yake mitano ijayo. Hoffenheim iko katika nafasi ya 14 hivi sasa baada ya mwishoni mwa juma kuizaba Eintracht Frankfurt kwa mabao 2-0 ikiwa ugenini.
Werder Bremen ambayo inaikabili Borussia Dortmund wiki ijayo imo katika hali mbaya ya kushuka daraja kwa msimu wa pili mfululizo baada ya kuporomoka hadi nafasi ya 16 baada ya kuchapwa mabao 2-1 na Augsburg , timu nyingine iliyoko katika hatari ya kushuka daraja.
Augsburg haijajinasua kutoka katika hatari hiyo licha ya kupanda hadi nafasi ya 14 , ikiwa na poimti 31 mbili tu nyuma ya Werder Bremen yenye pointi 28.
Hannover licha ya kutoka sare na Hertha Berlin ya mabao 2-2 inashikilia mkia ikiwa na pointi 18 na itakuwa miujiza iwapo itatoka katika janga hilo msimu huu.
Ingolstadt timu iliyopanda daraja msimu huu imejihakikishia pointi za kuibakisha katika daraja la juu baada ya kuiangusha Borussia Moengchengladbach kwa bao 1-0 nyumbani ,na kutibua mipango ya Gladbach kucheza katika Champions League msimu ujao.
Mwandishi: Sekione Kitojo / rtre / afpe / dpae / ZR
Mhariri: Iddi Ssessanga