1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Bayern yapata kipigo cha pili msimu huu dhidi ya Leipzig

Sekione Kitojo
19 Machi 2018

BVB imo katika  njia  kuelekea kucheza  Ulaya,  Leipzig  yaipa Bayern Munich  kipigo cha  pili  msimu  huu ,  FC Kolon yafufua  matumaini  ya  kubakia  katika  Bundesliga,

Bundesliga Leipzig gegen Bayern München - 2:1
Picha: picture-alliance/dpa/S. Stache

Borussia  Dortmund  ilijiimarisha  katika  nafasi  ya  tatu  ya msimamo  wa  ligi  ya  Ujerumani  Bundesliga  baada  ya  kupata ushindi  mwembamba  lakini  muhimu  dhidi  ya  Hannover 96 na kufikisha  pointi 48, baada  ya  kupata  ushindi  wa  bao  1-0 jana Jumapili.

Michy Batshuayi (katikati) akishangiria bao lake la ushindiPicha: imago/Kirchner-Media/D. Inderlied

Baada  ya  kutolewa  na  RB Salsburg  ya Austria katika mashindano  ya Europa  League katikati  mwa  juma lililopita , Borussia  Dortmund  ilionekana  kuwa  na  nia  ya  kutaka  ushindi tangu  mwanzo  wa  mchezo  na  ilifanya hivyo baada  ya mshambuliaji  wake Michy Batshuayi  kuuweka  mpira  wavuni,  ikiwa hilo  ni  bao  lake  la  6  katika  michezo 7  ya  Bundesliga  tangu ajiunge  na  kikosi  hicho kutoka  Chelsea ya  mjini  London  kwa mkopo.

Bayern ikipambana na RB LeipzigPicha: Reuters/M. Rietschel

Huyu  hapa nahodha wa  Borussia  Dortmund Marcel Schmelzer:

"Nafikiri, tumeona, kwamba  tumeonesha tunataka kushinda na  hilo tumelionesha  katika  kipindi  cha  kwanza  bila  shaka. Katika  kipindi cha  pili  kila  mmoja  wetu alipungukiwa  na  nguvu na  ndio  sababu tunafurahi, kwamba kwa sasa  tutapumzika  kwa  wiki  mbili."

Bayern Munich  ilipoteza  mchezo  wake  wa  pili  msimu huu  chini ya  kocha  Jupp Heynckes  jana  Jumapili  dhidi  ya  RB Leipzig, licha ya  kwamba kipigo  hicho  hakitaathiri  mwendo  wa  timu  hiyo kuelekea ubingwa  wake  mara  ya  6  mfululizo. Kocha  Jupp Heynckes  hajashitushwa  sana  na  kipigo  hicho  lakini  mlinzi Mats Hummels  alionya kwamba  timu  hiyo  inapaswa  kucheza  vizuri zaidi  katika  michuano  inayokuja  ya  Champions  League  katika duru  ya  robo  fainali.

Bayern Munich  inapambana  na  sevilla  ya  Uhispania  katika mchezo  wa  robo  fainali  ya  Champions League. Bayern inauwezo wa  kupandisha  kiwango  chake inapohitajika lakini  kipigo  cha  jana Jumapili  bila  shaka  kitachelewesha  sherehe  zake  za kutawazwa  mabingwa  katika  Bundesliga.

Yusuf Poulsen akipambana na Mats Hummels wa Bayern Munich(kulia)Picha: Reuters/M. Rietschel

Bayern yapata  kipigo

Bayern  itaikaribisha Borussia  Dortmund  katika  mchezo  ujao  Machi  31, lakini itatawazwa  mabingwa  mara  ya  6  mfululizo  iwapo Schalke 04 inayoshika  nafasi  ya  pili  haitaweza  kuishinda  Freiburg siku  hiyo.

Kipigo  hicho  cha  kwanza  mwaka  huu  cha  mabao 2-1  dhidi  ya RB Leipzig kimeipandisha  timu  hiyo  ya  mjini  Leipzig  hadi  katika nafasi  ya  6  ikiwa  na  pointi 43. Mshambuliaji  wa  RB Leipzig Timo Werner anazungumzia  utamu  wa  ushindi  dhidi  ya  Bayern.

"Wakati ukifunga  bao  dhidi  ya  Bayern  inafurahisha  sana. Na iwapo  mnashinda  dhidi  ya  bayern  inapendeza  zaidi. Leo tumecheza  vizuri  sana. Tulikuwa tunacheza  kwa  nguvu, na hatukuwaruhusu  Bayern  kuandaa  mchezo  wao. Na hii ni  lazima kusema.  Tulikuwa  nyuma  kwa  bao 1-0  dhidi  ya  Bayern  na tulibadilisha  matokeo  hayo, katika  mtindo , ambao  timu  bora kabisa  inavyofanya. Kwa  hilo  tunastahili  kujisikia  fahari."

Eintracht  Frankfurt  inapiga  hatua  kuelekea  kucheza  katika Champions League  ama  katika  Europa  League, na  kila  mchezo inaonesha  ukomavu  na  mbinu  za  hali  ya  juu  kuweza  kubakia katika  nafasi  hiyo. Frankfurt  chini  ya  kocha  Nico Kovac imeimarika  katika  nafasi  zote  na  iliibwaga  Mainz 05  kwa  mabao 3-0  siku  ya  Jumamosi  na  kujiimarisha  katika  nafasi  ya  nne ikiwa  na  pointi 45.

Kyriakos Papadopoulos wa Hamburg SVPicha: Getty Images/Bongarts/S. Franklin

Timu   ya  Hamburg  SV  ambayo  haijawahi  kushuka  daraja  tangu pale  Bundesliga  ilipoanzishwa  mwaka  1963 imeonekana  msimu huu  kuparaganyika  kabisa, na  sio  uwanjani  tu  hata  nje  ya uwanja.

Hamburg yasambaratika

Mlinzi Papadopolus baada  ya  kulalamikia  uongozi  wa timu  hiyo  ameweka nje  ya  uwanja  na  pia  mchezaji  wa  kati Mbrazil Walace  nae aliondolewa  kutoka  katika  kikosi  hicho kutokana  na  utovu  wa  nidhamu.

Matokeo  ya  mchezo  wa  27  wa  Bundesliga  hayakuwa  mazuri pia  kwa  timu  hiyo  pale  ilipokubali  kipigo  cha  mabao 2-1 nyumbani  dhidi  ya  Hertha  Berlin  na  hatimaye  kuchungulia mlango  wa  kuelekea  daraja  la  pili  ambapo  timu  hiyo  imebakia na  pointi 18 , na  ikiwa  ya  mwisho  kabisa.

Hali  hiyo  imekuja  baada  ya  majirani  zao  katika  msimamo  wa ligi  FC Kolon  kupata  ushindi  wa  kishindo  wa  mabao 2-0 dhidi  ya mahasimu  wao  wa  jadi  Bayer Leverkusen  jana  mjini  Kolon.

Wachezaji wa FC Kolon wakishangiria ushindi dhidi ya Bayer LeverkusenPicha: imago/U. Kraft

FC Koln imefikisha  sasa  pointi  20 mbili  juu  ya  Hamburg  ikiwa katika  nafasi  ya  17 na  ikijaribu  kuivuta  chini  Mainz 05  yenye pointi  25. Kolon  imefufua  matumaini  yake  ya  kubakia  katika daraja  la  kwanza  kwa  kucheza  mchezo  safi  wenye  ushindani dhidi  ya  Bayer  Leverkusen  na  kutoka  uwanjani  kifua  mbele katika  mchezo  huo  wa  watani  wa  jadi.

Huyu  hapa mlinda  mlango  wa  FC Kolon  Timo Horn.

"Bila  shaka  hii  inatufanya  tujisikie  vizuri. Tunajitahidi  kwa  kweli kufanya  kila  kitu. Nafarijika  kuona  kwamba  tumeshinda michezo miwili  ya  Derby  hapa  nyumbani. Hakuna  mtu anaweza  tena kuondoa  hilo, hata  kama  mwishoni  itakuwaje."

 

Mwandishi: Sekione  Kitojo / afpe / dpae / rtre

Mhariri: Mohammed Khelef

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW