Bayern yapata uhakika kunyakua ngao ya ubingwa mara ya nane
8 Juni 2020Ikiwa ni michezo minne tu imebakia kabla ya kumalizika kwa ligi, na na ni dhahiri pengo hili haliwezi kuponyoka mkononi. Hii ilionekana wazi tangu ushindi wa Bayern katika mpambano wa vigogo BVB dhidi ya Bayern karibu wiki mbili zilizopita. Mchezo huo ulileta matumaini kwa wapinzani wa Bayern kwamba huenda ikapoteza pointi na kufanya mbio za kuelekea ubingwa kuwa za mvutano. Matumaini haya yaliporomoka. Hata Bayer Leverkusen , ambao siku ya Jumamosi walianza kwa kushambulia sana lakini wakiwa wanafanya makosa kadhaa na upande wa ulinzi kukiwa wazi mno, hawakuweza kuwa kizingiti kwa Bayern. Bayern ilishinda kwa kishindo mabao 4-2.
Huyu hapa kocha wa Bayern Hans Flick.
"Katika soka suala muhimu ni kwamba lazima ushinde mchezo. Hicho ndicho tulichokionesha katika mwaka huu 2020. Timu hailegezi kamba. Leo pia imerudi katika hali ya kawaida baada ya mwanzo wenye matatizo, ambapo Leverkusen walitangulia kwa bao 1-0. Kama ilivyokuwa katika kipindi cha kwanza, tulionesha uwezo wetu, katika kipindi cha pili, lakini pia mpangilio na dhamira. Kwa hilo nimefarijika sana. Kwetu sisi kitu cha kwanza ni kwamba tunataka ubingwa. Kuna michezo minne iliyobaki. Hilo ndio lengo letu, na chochote kingine hakina maana."
Na hata katika msimu ujao kuna matumaini yasiyo na mipaka, kuhusiana na ubingwa wa tisa wa Bayern mfululizo. Bayern imejiimarisha kwa kumpatia mkataba wa kudumu kocha Hans Flick, pamoja na mlinda mlango mahiri Manuel Neuer, mshambuliaji Thomas Mueller na Alphonso Davies. Na Robert Lewandowski kila mmoja anafahamu kuwa ni mshambuliaji bora kabisa wa Bundesliga na pia mshambuliaji anayetarajiwa kujiunga na mabingwa hao kutoka Manchester City Leroy Sane. Kwa kikosi hicho, kuna uwezekano ubingwa ukawa mali ya Bayern kwa muda mrefu katika Bundesliga.
Pamoja na hayo katika Bundesliga Wolfsburg imepanda, Bremen imeporomoka , Schalke inazidi kudidimia. Katika michezo ya mwishoni mwa juma jana Jumapili . Bao la dakika za mwisho kwa kichwa la Wout Weghorst liliipa Wolfsburg ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Werder Bremen na kuimarisha nafasi yake ya kucheza katika kikombe cha ligi ya Ulaya na kupandikiza mbinyo mkubwa dhidi ya wenyeji Bremen ambao wana hofu ya kutumbukia katika daraja la pili.
Kocha wa Werder Bremen Florian Kohfeldt hajakata tamaa:
"Kwa mara nyingine tena tumetoka patupu. Inakera sana, kwa msingi wa matokeo ya jana. Tunapaswa kujinyanyua na kujifuta baada ya kuanguka, na kisha katika michezo minne iliyobakia kujaribu kila tulichonacho, ili tufikie katika nafasi ya mchujo. Kuhusu hilo bado nina matumaini, kwasababu naamini, timu leo haijacheza kama maiti, tulishuhudia timu, ikipambana, ikijituma, na wachezaji kukimbia kila mahali, hadi dakika ya mwisho, tulipobaini kwamba haiwezekani tena. lakini sifikiri kwamba itatokea tena."
Bremen kwa sasa iko nafasi ya 17 ikiwa na pointi 25, pointi 3 nyuma ya Dusseldorf iliyoko katika nafasi ya 16 ya mchujo.
Union Berlin iliyopanda daraja msimu huu imesogea karibu na eneo la usalama katika msimamo wa ligi katika msimu wake wa kwanza wa Bundesliga kwa kupata sare ya bao 1-1 nyumbani dhidi ya Schalke 04, ambayo sasa imefikia rekodi yake ya ndani ya michezo 12 bila ushindi. Kwanini Schalke imerejea baada ya mapumziko ya corona katika hali dhaifu huyu hapa kocha wa Schalke David Wagner:
"Unapokuwa uko nyuma kwa kufungwa bao, kwa mara nyingine tena kutokana na makosa makubwa ya mchezaji, na kisha ukapambana katika mchezo kama huo na kusawazisha, katika kipindi kigumu kabisa, kama tulichomo kwa sasa, unaweza kimsingi kufanya subira tu, kwamba vijana waweze kujiamini na kupambana. Na nafikiri , hicho ndio walichofanya. Wamejaribu. Niseme wazi hata hivyo , kwamba katika hali ya sasa ukomo wetu unaonekana katika kucheza kandanda."
Augsburg ilitoka sare ya bao 1-1 dhidi ya FC Koeln . Borussia Dortmund ilipata ushindi mwingine siku ya Jumamosi nyumbani kwa kuishinda Hertha BSC Berlin kwa bao 1-0 na kujiimarisha katika nafasi yake ya pili. RB Leipzig ilishindwa kutamba mbele ya SC Paderborn nyumbani kwa kutoka sare ya bao 1-1 na Dusseldorf na TSG Hoffenheim zilitoshana nguvu kwa kufungana mabao 2-2.
Timu nne zaidi za Bundesliga zilipiga goti kabla ya michezo yao jana Jumapili. Borussia Dortmund na Hertha Berlin zilipiga goti kwanza kabla ya mchezo wao siku ya Jumamosi katika ishara ya kupinga ubaguzi kufuatia maandamno dhidi ya ukatili wa polisi na ubaguzi nchini Marekani kuhusiana na mauaji dhidi ya George Floyd mjini Minneapolis siku ya Mei 25.
Wolfsburg na Werder Bremen walifuatia , Union Berlin na Schalke, nazo zikafuatia.