1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Bayern yarejea katika ushindi, Borussia yaangukia pua

Sekione Kitojo
16 Oktoba 2017

Jupp Heynckes kocha  wa Bayern Munich awarejesha mabingwa watetezi wa Bundesliga katika  njia ya ushindi. Ujerumani  yaendelea  kushikilia nafasi ya kwanza katika orodha ya  timu bora za FIFA.

Bundesliga: Bayern München gegen SC Freiburg
Wachezaji wa Bayern Munich , Kimmich(katikati)Coman, na Robben Picha: Imago

Bayern Munich imerejea  tena  katika  njia  ya  ushindi  baada  ya kubadilisha  kocha  wake  Carlo Ancelotti wiki  mbili  zilizopita  na kumpa  kazi  hiyo  kocha  wake mzoefu Jupp  Heinckes , na  kama alivyo  daktari  bingwa , aliweza  kutambua  matatizo  yako  wapi na kukipa makali  ya  wembe  kikosi  chake  na  kuinyoa  Freiburg  kwa mabao 5-0  katika  mchezo  wake  wa  kwanza  kukaa  katika  benchi la  ufundi . Heynckes  alistaafu  katikati  ya  mwaka  2013  baada  ya kuipatia  Bayern Munich mataji  matatu  katika  msimu  mmoja, Champions League, ubingwa  wa  ligi  na  kombe  la  Shirikisho DFB Pokal.

Thomasd Mueller wa Bayern MunichPicha: picture-alliance/M.Ulmer

Mshambuliaji  wa  Bayern Munich na  nahodha  wa  sasa  wa  timu hiyo Thomas Mueller  amesema  matokeo  hayo  yamewapa motisha zaidi  ya  kufanya  vizuri zaidi.

"Tunapaswa  kuendelea hivi  hivi. Bila  shaka tulicheza  vizuri , lakini katika  mchezo  wa  mpira , mchezo  muhimu  kila  mara  ni ule unaofuatia. Tumefanya kazi  nzuri, tuliweza  kubadilisha mchezo wetu  kabisa, lakini  pia  kuna  mambo  fulani  lazima  tuyafanyie kazi. Bila  shaka  matokeo  haya  yanatupa nguvu zaidi na  yatupasa kuendelea hivi hivi."

Bayern Munich  imesogea  hadi  nafasi  ya  pili  nyuma  ya  Borussia Dortmund  ikiwa  na  pointi 17 , pointi  2  nyuma  ya  viongozi  hao wa  Bundesliga, ambao  waliangukia  pua  siku  ya  Jumamosi  katika mchezo maalum  wa  siku  dhidi  ya  RB Leipzig. Katika  jioni  hiyo RB Leipzig  ilivunja  rekodi  mbili  za  Dortmund , kutofungwa nyumbani  katika  Bundesliga  kwa  michezo 41, na  pia  timu  hiyo inayoongozwa  na  kocha  Ralph  Hasenhuettl  ilifikisha  mwisho rekodi  ya  Dortmund  ya  kutofungwa  msimu  huu.

Picha: picture-alliance/B.Thissen

Borussia Dortmund hoi kwa RB

RB Leipzig iliishindilia  Borussia  Dortmund  mabao 3-2  nyumbani, na  kwa mara  nyingine  tena  kuweka  wazi  ubovu  wa  safu  ya  ulinzi  ya Borussia Dortmund, ambao  umeonekana  wazi  katika  michezo yake  katika  ligi  ya  mabingwa  wa  Ulaya  Champions League  , dhidi  ya  Totteham Hot Spurs  na  pia  dhidi  ya  Real Madrid.

Mshambuliaji wa Borussia Dortmund Pierre-Emerick Aubameyang akiwa anatafakari kufungwa na RB LeipzigPicha: Getty Images/L.Baron

FC Kolon imebakia  bila  ushindi  msimu  huu na  inakalia  nafasi  ya mwisho  katika  msimamo  wa  ligi , baada  ya  kukubali  kipigo  cha mabao 2-1  nyumbani  kwa  VFB Stuttgart  siku  ya  ufunguzi  wa wiki  ya  nane  ya  bundesliga siku  ya  Ijumaa.  FC Kolon  bado  ina pointi  moja  tu  kibindoni  na katika  mchezo  wa  9  FC Kolon ina miadi  nyumbani  na  SV Werder  Bremen , moja  kati  ya  timu zilizoko  majirani  katika  msimamo  wa  ligi, wakati  Werder Bremen iko  nafasi  ya  17, FC Kolon  iko  nafasi  ya  18.

Nani  anaondoka na  pointi  tatu  muhimu ni  swali  la  kungoja  na  kuona.  Kocha  wa Bremen  Alexander Nouri yuko  katika  mbinyo  mkali  wa  kuleta mafanikio  katika  kikosi  hicho, ama  sivyo  kibarua  kitaota  majani. Kinyume  na  mwenzake  wa  Kolon Peter Stoeger , anaungwa mkono  kwa  asilimia  100  na  viongozi  wa  klabu  pamoja  na mashabiki.

Werder  Bremen imetumbukia  katika  hali  hiyo  ngumu  baada  ya jana  kupokea  kipigo  cha  mabao 2-0  dhidi  ya  Borussia Moenchengladbach, ambayo  imepanda  hadi  katika  nafasi  ya tano  katika  msimamo  wa  ligi.

Kocha  Dieter  Hecking wa  Gladbach anasema.

Wachezaji wa Borussia Moenchengladbach wakipongezana baada ya kupata bao dhidi ya Werder BremenPicha: Getty Images/M.Rose

"Ilikuwa  ushindi usio  na  shaka, tulistahili  kushinda kwa  kiasi kikubwa.  Tungeweza  pia  kupata bao  ama  mabao  zaidi katika mchezo  huo. Lakini jinsi gani  na  vipi  timu iliweza  kushinda  kwa kweli  ilikuwa  vizuri  sana."

Hamburg SV  pia  imo  katika  hali  mbaya  iliishia  kushika  nafasi  ya 15 , baada  ya  kupokea  kipigo  cha  mabao 3-2  dhidi  ya  Mainz 05 siku  ya  Jumamosi.

Bayer Leverkusen yaendelea kufanya vibaya

Mwanzo  mbaya  wa  Bayern Leverkusen  katika  msimu  huu  wa  ligi umendelea jana  Jumapili , ambapo  ilishindwa  mara  mbili  kulinda ushindi  wake  dhidi  ya  Wolfsburg.  Na Leverkusen ilijikuta  ikikubali sare  ya  mabao  2-2  dhidi  ya  VFL  Wolfsburg licha  ya  kwamba sare  hiyo  haijasaidia sana  timu  hizo  ambazo  ziko  nafasi  ya  12 na  14 zikitengana  kwa  pointi moja  tu. Lakini  hali  hiyo haijamkosesha  raha  sana  kocha  mpya  wa  Wolfsburg  Martin Schmidt ambaye  anasema amefarijika  kupata  sare.

"Tumetoka  uwanjani  mara  tano  bila  ya  kufungwa, hii  ina  maana pia  kwamba  hatuachii mwanya hata kidogo. Hata tukiwa  tuko nyuma  tunapambana  na  kurudisha mabao.  Hali  hiyo ikiendelea kuwapo kichwani, na  mafanikio ya pointi tatu pia  yanafuatia."

Lakini  kwa  kocha  wa  Bayern 04  Leverkusen  Heiko Herrlich haikuwa  ni  matokeo yanayoridhisha.

Wachezaji wa Bayer Leverkusen wakishangiria bao lao dhidi ya wolfsburgPicha: Getty Images/P.Stollarz

Heiko Herrlich (Bayer 04 Leverkusen)

"Leo tulitaka  kushinda na iwapo tungetumia  nafasi zilizopatikana tungetoka  uwanjani  tukiwa  washindi. Lakini  haikuwezekana  na kwa  kweli  inakera."

Ushindi  wa  mabao 2-0  wa  Schalke 04  dhidi  ya  Hertha BSC Berlin  umeiweka  timu  hiyo  katika  nafasi  ya  6 na  Eintracht Frankfurt  iliishinda Hannover 96 kwa  mabao 2-1  na  kuchupa  hadi nafasi  ya  7.

Wachezaji wa Wolfsburg wakirejea kati baada ya kupata bao dhidi ya LeverkusenPicha: Getty Images/L.Baron

Na  Ujerumani imeendelea  kukalia  nafasi  ya  juu  ya  orodha  ya timu  bora  duniani  kwa  sasa iliyotolewa  na  shirikisho  la kandanda  duniani  FIFA  kama  ilivyochapishwa  leo  Jumatatu na kuthibitisha  timu  za  kiwango  cha  juu  zitakazowekwa  katika chungu  kimoja  katika  upangaji  wa timu zitakazoshiriki  katika makundi  ya  fainali  za  kombe  la  dunia mwakani , pamoja  na michuano  ya  mchujo  ya  kombe  la  mataifa  ya  bara  la  Ulaya.

 

Mwandishi: Sekione Kitojo / afpe / rtre / dpae / ape

Mhariri: Mohammed  Abdul-Rahman

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW