Bayern yarejea kileleni mwa Bundesliga
24 Septemba 2014Munich pia imechupa na kuipita Hoffenheim na Mainz 05, timu ambazo zote zimeridhika na sare na kurejea nyuma kwa pointi mbili nyuma ya Bayern wakati Schalke 04 imepata ushindi wake wa kwanza msimu huu.
Munich haikusubiri muda mrefu kuweza kupachika bao, ikichukua uongozi katika mchezo huo baada ya dakika nane kwa pasi safi. Arjen Robben alimmegea pasi Thomas Mueller , ambaye aliugonga mpira kwa kisigino na kumfikia Mario Goetze ambaye hakufanya makosa na kuuweka mpra wavuni.
"Tulikuwa tumejitayarisha sana na mchezo huu. Tulitaka kufanya vizuri kutoka mchezo wetu wa mwisho," amesema Goetze , akimaanisha sare ya bila kufungana kati ya Bayern Munich na Hamburg mwishoni mwa juma lililopita.
Wanaoiwinda Bayern wachemsha
Hoffenheim imepoteza nafasi ya kuifuatia Munich lakini Jannik Vestergaard alifunga bao dakika tatu katika muda wa majeruhi na kuiwezesha timu yake kupata sare ya mabao 3-3 nyumbani dhidi ya SC Freiburg na kuifikisha timu hiyo katika pointi tisa.
Jonas Hofmann aliipa Mainz 05 uongozi katika mchezo dhidi ya Eintracht Frankfurt na Shinji Okazaki alipata bao lake la tano msimu huu katika dakika ya 44.
Lakini Alexander Maier alipunguza pengo kwa Frankfurt dakika chache kabla ya kuanza dakika za majeruhi kabla ya Seferovic kuweka salama point moja kwa Frankfurt.
Ushindi wa kwanza wa Schalke msimu huu
Schalke imepata pointi zake tatu za kwanza msimu huu baada ya kuikandika Werder Bremen kwa mabao 3-0.
Tulikuwa na mbinyo mkubwa mno mwanzoni mwa mchezo huu. Lakini tulicheza vizuri katika kipindi cha pili," amesema kocha wa Schalke Jens Keller, ambaye hakuweza kupata huduma ya mchezaji wake wa kati Julian Draxler na Kevin-Prince Boateng ambao wana kadi nyekundu.
Leo (24.09.2014) ligi hiyo inaendelea ambapo Bayer Leverkusen inaweza kuchupa kutoka nafasi ya tano hadi ya pili iwapo itafanikiwa kuikaba koo FC Augsburg inayotembelea mjini Leverkusen.
Borussia Dortmund pia inaingia dimbani leo , ikiwa nyumbani dhidi ya VFB Stuttgart, wakati Borussia Moenchengladbach inaikaribisha Hamburg SV, VFL Wolfburg iko njiani ikiifuata Hertha Berlin na Hannover 96 inaikaribisha FC Kolon.
Mwandishi: Sekione Kitojo / afpe
Mhariri: Mohammec Khelef