Bayern yashinda mchezo wa ufunguzi wa Ligi ya Bundesliga
27 Agosti 2018Ligi ya Bundesliga imerejea tena dimbani kwa msimu wa 56 wa mwaka 2018 / 19, ambapo mabingwa watetezi Bayern Munich wanatetea taji lao kwa mara ya saba mfululizo ilipata ushindi katika mchezo wao wa kwanza katika uwanja wa Allianz Arena mjini Munich kwa kuikandamiza TSG Hoffenheim kwa mabao 3-1 siku ya Ijumaa.
Hapo jana Jumapili mzunguko wa kwanza ulimalizika kwa Mainz 05 kuikandika VFB Stuttgart kwa bao 1-0, na katika mchezo wa mwisho Borussia Dortmund iliibamiza RB Leipzig kwa mabao 4-1.
Kurejea kwa kocha Lucien Favre katika Bundesliga kumeanza kwa kishindo wakati kikosi chake cha Dortmund kikimaliza washindi katika mchezo huo dhidi ya RB Leipzig, lakini kocha huyo raia wa Uswisi alikiri kwamba matokeo hayo ni ya juu mno kuliko mchezo huo ulivyokuwa.
"Kuna mengi ya kuweka sawa," amesema Favre baada ya kukiangalia kikosi chake kikichapwa bao la haraka sekunde 31 lakini kilijibu kwa mabao matatu ya haraka haraka katika kipindi cha kwanza mbele ya mashabiki 80,000 katika uwanja wa Signal Iduna Park mjini Dortmund.
Makamu bingwa lakini Schalke 04 ilikubali kipigo katika mchezo huo wa kwanza mbele ya VFL Wolfsburg kwa mabao 2-1 katika mchezo ambao ulikuwa ni wa kasi na wa vuta nikuvute. Frankfurt ilipiga hatua moja mbele baada ya kuiangusha Freiburg kwa mabao 2-0 , wakati timu mbili zilizopanda daraja Nuremburg na Dusseldorf zilikaribisha kwa vipigo , wakati Nuremburg ikipokea kipigo cha bao 1-0 dhidi ya Herha Berlin , Dusseldorf ilitandikwa mabao 2-0 na Augsburg.
DW ilikuwapo uwanjani kushuhudia mpambano kati ya Wolfsburg na Schalke , kama anavyosimulia Josephat Charo.
Mwandishi: Sekione Kitojo / ape / afpe / rtre / dpae
Mhariri: Mohammed Abdul Rahman