1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Bayern yavunja rekodi kwa kishindo

13 Aprili 2026

Bayern Munich imefikia mabao 105 msimu huu. Musiala, Goretzka na wenzake waliongoza maangamizi huku Kompany akisema kikosi chake “hakijamaliza kazi,” na Bayern ikikaribia kutawazwa mabingwa wiki ijayo.

 FC Bayern München
Rekodi ya muda mrefu iliwekwa na kikosi kilichojumuisha magwiji wa klabu kama Franz Beckenbauer, Gerd Müller na Uli Hoeness.Picha: Ibo Ot/AFP

Bayern Munich ilipata ushindi mnono wa 5–0 dhidi ya St. Pauli , ikivunja rekodi ya mabao ya Bundesliga iliyodumu kwa miaka 54 na kusogea karibu kutwaa taji lao la 35 la ligi.

Bao la Leon Goretzka dakika ya 53, ambalo lilikuwa la pili kwenye mchezo, liliifanya Bayern kufikisha mabao 102 msimu huu wa ligi, na kuvunja rekodi iliyowekwa na miamba hao wa Bavaria msimu wa 1971–72.

Rekodi hiyo ya muda mrefu iliwekwa na kikosi kilichojumuisha magwiji wa klabu kama Franz Beckenbauer, Gerd Müller na Uli Hoeness.

Kocha wa Bayern, Vincent Kompany, amesema alijua kikosi chake kingevunja rekodi hiyo.

"Nilimuona Uli Hoeness jana na nikamwambia ‘Tunakuja kwa ajili ya rekodi.' Rekodi hii imekuwepo kwa muda mrefu na wachezaji wanaweza kujivunia, lakini tunaendelea kusonga mbele,” Alisema Kompany

Mfungaji bora Harry Kane alianza akiwa benchi, lakini Jamal Musiala, Michael Olise, Nicolas Jackson na Raphael Guerreiro waliungana na Goretzka kwenye orodha ya wafungaji, huku Bayern ikijitanua kwa tofauti ya pointi 12 dhidi ya Borussia Dortmund, waliopoteza kwa Bayer Leverkusen mapema Jumamosi.

Ikiwa zimesalia mechi tano msimu huu, mabingwa watetezi Bayern wanaweza kutwaa taji mapema wiki ijayo nyumbani dhidi ya Stuttgart.

Kwa kuzingatia mechi ya marudiano ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa dhidi ya Real Madrid Jumatano, Bayern pia ilianza bila Luis Díaz, Dayot Upamecano na Jonathan Tah, waliokaa benchi.

Kukosekana kwa nyota hao hakukuathiri chochote kwani Musiala aliwafungulia wageni dakika ya tisa kwa kichwa.

Mapema kipindi cha pili, Goretzka alifunga kutoka karibu na goli na kuvunja rekodi ya zaidi ya nusu karne.

Dakika moja baadaye, Olise akaongeza bao jingine. Jackson, aliyemrithi Kane, akafunga lake, na Guerreiro akahitimisha ushindi huo kwa kufikisha rekodi mpya ya mabao 105.

Andrich aiangusha Dortmund

Robert Andrich alifunga shuti la mbali mwishoni mwa kipindi cha kwanza na kuipa Leverkusen ushindi wa 1–0 ugenini, na kuwa timu ya pili tu kuifunga Dortmund msimu huu.

Dortmund, ambao walikuwa wamepoteza mara mbili tu msimu huu—mara zote dhidi ya Bayern—wamebaki nafasi ya pili kwa tofauti ya pointi nane licha ya mfululizo wao wa ushindi wa mechi nne kukatika.

Robert Andrich aliachia shuti kutoka mabli na kumuacha kipa Gregor Kobel hoi.Picha: Martin Meissner/AP Photo/picture alliance

Siku moja baada ya kuongeza mkataba wake hadi 2031, Nico Schlotterbeck alizomewa na baadhi ya mashabiki kufuatia taarifa kwamba kipengele cha kuuzwa kiliongezwa kwenye mkataba wake.

Mlinzi mwenzake, Waldemar Anton, alisema "Tuna furaha Schlotti amesaini mkataba mpya. Hakustahili kuzomewa . Hilo linaumiza timu, na mashabiki wanapaswa kuelewa hivyo. Ni upuuzi na hatuwezi kuukubali.”

Dortmund, ambao chini ya kocha Niko Kovac huwa waangalifu na wasiopenda hatari, walikuwa wakishambulia kwa ufasaha katika dakika 30 za mwanzo, lakini Andrich aliwazidi ujanja kwa urahisi.

Kiungo huyo wa Ujerumani aliukamata mpira uliopotezwa na Ramy Bensebaini, akachukua hatua moja na kupiga shuti la chini lililomshinda kipa Gregor Kobel.

Nafasi bora ya Dortmund ilikuja dakika saba kabla ya mwisho wakati Serhou Guirassy alipogonga upande wa chini wa mwamba baada ya kupokea pasi ya Carney Chukwuemeka.

Diomande awaheshimisha Leipzig

Katika mechi nyengine Yan Diomande aliipa RB Leipzig ushindi wa 1–0 dhidi ya Borussia Mönchengladbach, akiongeza matumaini ya kumaliza ndani ya nne bora.

Bao lake lilifanya Leipzig, walioko nafasi ya tatu, wajitanue kwa pointi tatu mbele ya Stuttgart, wanaocheza Jumapili dhidi ya Hamburg, huku Leverkusen wakiwa pointi moja nyuma nafasi ya tano.

Yan Diomande asifiwa kwa muendelezo mzuri RB Leipzig. Picha: Alex Grimm/Getty Images

Bao hilo liliendeleza msimu wa kuvutia wa kijana huyo mwenye miaka 19, ambaye sasa amefunga mabao 11.

Nahodha wa Leipzig, David Raum, alimsifu Diomande kama "mchezaji mwenye uwezo wa kiwango cha dunia.”

Mashabiki wa Gladbach walionyesha bango lililomlenga nahodha wao Rocco Reitz, atakayejiunga na Leipzig msimu ujao, likisema: "Anayetaka kilicho hapa hawezi kuwa nahodha wetu.”

Kwingineko, Wolfsburg walipoteza 2–1 nyumbani dhidi ya Eintracht Frankfurt na kuzidi kusogea karibu na kushuka daraja.

Mabao ya Oscar Højlund na Arnaud Kalimuendo yaliwaacha Wolfsburg, walioko nafasi ya pili kutoka mwisho na wameshinda mara moja tu katika mechi 14 za 2026, wakiwa pointi sita kutoka salama.

Timu ya mwisho, Heidenheim, iliendeleza matumaini yao madogo ya kusalia Bundesliga kwa ushindi wa 3–1 nyumbani dhidi ya Union Berlin.

Ushindi huo—wa kwanza tangu mapema Desemba—uliwafanya wasogee pointi mbili nyuma ya Wolfsburg na pointi nane kutoka Cologne walioko nafasi ya 15

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW