1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
JamiiUkraine

Bei ya chakula duniani ilifikia rekodi ya juu

6 Januari 2023

Data za Umoja wa Mataifa zimeonyesha kwamba bei ya chakula duniani ilishuka kwa mwezi wa tisa mfululizo katika mwezi wa Disemba lakini ikafikia kiwango cha juu zaidi katika rekodi kwa mwaka mzima wa 2022.

Bei ya vyakula ilipanda na kuvunja rekodi mnamo Machi baada ya Urusi kuivamia Ukraine, msambazaji mkuu wa ngano na mafuta ya kupikia duniani.

 soma FAO: Watu milioni 22 wanakabiliwa na ukosefu wa chakula Congo

Lakini bei zimeshuka tangu wakati huo, huku kukiwa na afueni zaidi iliyoletwa na makubaliano yaliyosimamiwa na Uturuki na Umoja wa Mataifa mwezi Julai ambayo yaliondoa kizuizi cha jeshi la wanamaji la Urusi kwenye mauzo ya nafaka ya Ukraine.

Shirika la Chakula na Kilimo Ulimwenguni, FAO, limesema Ijumaa ya leo kwamba faharasa yake ya bei, ambayo inafuatilia mabadiliko ya kila mwezi ya bei kwa bidhaa za chakula kimataifa, ilishuka hadi nukta 132.4 mwezi Desemba, punguzo la asilimia 1.9 kutoka hali ilivyokuwa mwezi Novemba. Pia ilikuwa chini kwa asilimia moja kuliko Disemba 2021.

soma Umoja wa Mataifa wasema hatua ya kwanza yafikiwa katika kuwezesha nafaka kusafirishwa kutoka Ukraine.

Lakini kwa upande mwengine, faharasa hiyo ilipanda juu kwa asilimia 14.3 ya juu kwa jumla mwaka wa 2022 ikilinganishwa na mwaka uliopita kwani ilifikia kiwango cha juu cha alama 143.7.

Bei ya bidhaa

Picha: Abdullah Momin

Kulingana na mwanauchumi mkuu wa shirika la FAO, Maximo Torero, kutangamaa kwa bidhaa za chakula kunashuhudiwa baada ya miaka miwili ya hali ngumu, ingawa alionya kwamba bado vyakula vikuu vingi viko katika bei ya juu, huku bei ya mchele ikipanda na kwamba bado kuna hatari nyingi zinazohusiana na ugavi katika siku zijazo.

Bei ya mahindi duniani ilikuwa juu kwa asilimia 24.8 kwa wastani mwaka 2022 kuliko mwaka 2021, huku ngano ikiwa ghali zaidi kwa asilimia 15.6, lakini bei ya mahindi ilishuka mwezi Disemba, hasa kutokana na "ushindani mkubwa" kutoka Brazil, kwa mujibu wa shirika hilo.

Ngano pia ilipungua kwa mwezi huo na mavuno yanayoendelea katika mataifa ya kusini yameongeza usambazaji na hivyo kuzidisha ushindani kati ya wauzaji bidhaa za nje.

Bei ya mafuta ya kupikia ilifikia rekodi mpya ya juu mnamo 2022 lakini ilishuka kwa asilimia 6.7 mwezi kwa mwezi Desemba hadi kiwango chake cha chini zaidi kuwahi kushuhudiwa tangu Februari 2021.

Shirika hilo la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa limesema pia bei za maziwa na nyama zilifikia viwango vyao vya juu zaidi tangu 1990, huku nyama ikishuka kwa asilimia 1.2 mnamo Desemba, lakini maziwa yakipanda kwa asilimia 1.1 kwa mwezi huo.

 

//AFP