Beijing. Korea ya kaskazini yakubali kuzima vinu vyake vya kinuklia.
4 Oktoba 2007Korea ya kaskazini imeidhinisha makubaliano ya kusitisha kabisa vinu vyake vyote vya kinuklia ifikapo mwishoni mwa mwaka huu kwa mujibu wa shirika la habari la China linalomilikiwa na serikali.
Makubaliano hayo yanatoa muda maalum kwa Korea ya kaskazini kuonyesha mipango yake yote ya kinuklia na kuzima kabisa vinu vya kinuklia ili kuweza kupata tani za ujazo 950,000 za mafuta ama msaada unaolingana na thamani ya tani za mafuta hayo. Wajumbe wa majadiliano wamefikia makubaliano hayo katika muswada wa mpango mjini Beijing siku ya Jumapili baada ya siku nne za majadiliano baina ya Korea zote mbili, China, Japan , Russia na Marekani . Katibu mkuu wa umoja wa mataifa Ban Ki-moon amekaribisha tamko hilo na kusema kuwa ni hatua muhimu kuelekea juhudi za kidiplomasia katika kuliweka eneo la rasi ya Korea kutokuwa na silaha za kinuklia.