Beijing iliipiku Almaty ya Kazakhstan
31 Julai 2015Hivyo, Beijing umekuwa mji wa kwanza kupewa kibali cha kuandaa Michezo ya Olimpiki ya majira ya joto na baridi. Shangwe na vifijo vilitawala mjini Beijing baada ya Rais wa IOC Thomas Bach kutangaza uamuzi huo
Mji huo mkuu wa China umeupiku mji wa Almaty wa Kazakhstan katika kura ya siri iliyopigwa na wanachama 85 wa IOC iliyoandaliwa katika mkutano wa Kuala Lumper. Kura hiyo ilipigwa mara mbili, kwanza kwa njia ya elektroniki na kisha kwa karatasi baada ya kugundulika kuwa mfumo wa elektroniki ulikuwa na dosari. Liu Yandong ni naibu waziri mkuu. Alisema "kukubaliwa ombi letu kuna maana ya mwanzo mpya. Tutafanya kazi kulijenga taifa letu, na kuwa nchi bora zaidi, ili tuweze kuupa ulimwengu Michezo murwa kabisa na ya kufana”.
Beijing ilipata kura 44 dhidi ya 40 ambapo Rais wa IOC Thomas Bach hakupiga kura yake. Uamuzi huo hata hivyo umezusha shutuma kutoka kwa wanaharakati wa haki za binaadamu. Beijing ilipigiwa upatu kupewa kibali hicho kwa sababu tayari ilidhihirisha hilo wakati ilipoandaa Michezo ya Olimpiki ya msimu wa joto mnamo mwaka wa 2008.
Mwandishi: Bruce Amani/AFP/Reuters/AP/DPA
Mhariri: Mohammed Khelef