BEIJING: Makubaliano yafikiwa kuhusu mpango wa nyuklia
13 Februari 2007Wajumbe katika mazungumzo ya mataifa sita kuhusu mpango wa nyuklia wa Korea Kaskazini wanaonekana wamefikia makubaliano hivyo kumaliza mkwamo wa miaka mitatu ya mazungumzo hayo.
Mjumbe wa Marekani katika mazungumzo hayo, naibu waziri wa mambo ya nje, Christopher Hill, alitangaza baada ya mazungumzo yaliyodumu muda wa saa 16 kwamba makubaliano ya kwanza yamefikiwa. Marekani haijayapa uzito makubaliano hayo.
Bwana Hill amesema alipata ushauri kutoka kwa waziri wa mashauri ya kigeni wa Marekani Bi Condoleezza Rice.
´Nilizungumza na waziri Condoleezza Rice jana usiku mara nyingi na alikuwa akifuatilia kwa karibu mazungumzo yalivyokuwa yakiendelea. Bi Rice alinishauri katika misingi ya kuzingatia wakati.´
Rasimu ya makubaliano hayo inajumulisha ahadi za kupokonywa silaha na msaada wa nishati. Kamati zitaundwa ili kushughulikia hali ya wasiwasi ya kikanda.
Kufikia sasa Korea Kaskazini haijatoa matamshi yoyote rasmi kuhusiana na makubaliano hayo.
Afisa wa Korea Kusini amesema makubaliano hayo yatahitaji kuidhinishwa na serikali za kila taifa linalowakilishwa katika mazungumzo kuhusu mpango wa nyuklia wa Korea Kaskazini.