1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Beijing. Miito yatolewa kuwa na utulivu kutokana na hali ya wasi wasi kati ya China na Japan, baada ya maandamano yaliyoleta uharibifu wa mali.

20 Aprili 2005

Raia wa China wametakiwa na serikali ya nchi hiyo kuacha kufanya maandamano ya kuipinga Japan. Waziri wa mambo ya kigeni wa China Li Zhaoxing katika taarifa iliyosomwa katika vyombo vya habari nchini humo amesema kuwa Wachina hawapaswi kuhatarisha hali ya kijamii. Taarifa hiyo inakuja wakati mmoja na miito ya utulivu kutoka kwa mawaziri wengine wa mambo ya kigeni kutoka mataifa ya Asia walioko mjini jakarta wakijitayarisha na mkutano wa mataifa hayo na Afrika.

Waziri wa mambo ya kigeni wa Malaysia Syed Hamid Albar amesema kuwa hali hiyo ya wasi wasi kati ya mataifa hayo mawili yenye nguvu kubwa za kiuchumi katika Asia inatia wasi wasi.

Katika wiki za hivi karibuni waandamanaji walikuwa wakitupa mawe katika balozi na biashara za Wajapan , wakati waandamanaji wakipinga kuidhinishwa na serikali ya japan kitabu cha historia kitakachotumika mashuleni ambacho hakitilii maanani vitendo vya uharibifu na ukatili vilivyofanywa na Japan kabla na baada ya vita vikuu vya pili vya dunia.

Maafisa wa viwanda wa Japan na China wanasema hata hivyo kuwa biashara ya kila mwaka inayofikia kiasi cha dola bilioni 178 inaendelea licha ya hali hiyo ya wasi wasi.