BEIRUT : Lebanon yaomba wanamaji wa Ujerumani
5 Septemba 2006Ofisi ya Waziri Mkuu wa Lebanon Fouad Siniora imesema nchi hiyo itaiomba Ujerumani itume wanamaji wa kupiga doria kwenye mwambao wake wa bahari katika shughuli za kulinda amani za Umoja wa Mataifa nchini humo.
Ombi hilo ambalo kwayo serikali ya Ujerumani imekuwa ikilisubiri na ambalo halina budi kupitia Umoja wa Mataifa linakuja kwa sharti kwamba Israel inaondowa vikwazo vyake vya baharini kwa Lebanon.Serikali ya Lebanon pia inataka manowari za Ujerumani kuwa umbali wa kama maili saba kutoka fukwe zake.
Hata hivyo ombi hilo limechukuwa muda kutolewa katika baraza la mawaziri la Siniora ambalo lina mawaziri wawili kutoka kundi la Hizbollah.
Dhamira kuu ya kuwa na vikosi hivyo vya wanamaji kupiga doria ni kuzuwiya kusafirishwa kwa magendo kwa shehena ya silaha kwa kundi la Hizbollah.