Beirut. Majeshi ya Lebanon yapambana na wakimbizi wa Kipalestina.
21 Mei 2007Majeshi ya Lebanon yanapambana na wanamgambo katika kambi ya wakimbizi ya Wapalestina kaskazini ya nchi hiyo kwa muda wa siku ya pili mfululizo.
Kiasi watu 50 wameuwawa katika mapigano hayo, ambayo yamezuka baada ya polisi kuvamia jengo moja , wakitafuta watuhumiwa waliofanya uporaji katika benki moja.
Wanamgambo hao ni wanachama wa kundi lililojitenga la wapalestina la Fatah al-Islam, ambalo linadaiwa kuwa na mahusiano na al Qeda na watu wenye imani kali kutoka Syria.
Baraza la mawaziri la Lebanon limelishutumu kundi hilo la Fatah al-Islam kwa kujaribu kuidhoofisha serikali katika wakati umoja wa mataifa unajaribu kuunda mahakama ya kimataifa itakayowahukumu watuhumiwa wa mauaji ya mwaka 2005 ya waziri mkuu wa Lebanon Rafik Hariri.
Wakati huo huo , mtu mmoja ameuwawa na wengine 10 wamejeruhiwa katika mlipuko wa bomu katika eneo linaloishi Wakristo mashariki ya Beirut.