BEIRUT: Mashambulio ya Israel yaendelea nchini Lebanon
3 Agosti 2006Matangazo
Ndege za kivita za Israel mapema leo hii zimeshambulia tena vituo katika mji mkuu wa Lebanon,Beirut.Mashambulio ya angani yamelenga eneo la kusini la Beirut linalodhibitiwa na Hezbollah.Mashahidi wamesema mji wa Beirut ulitikiswa na kama miripuko mitatu,baada ya makombora kukipiga kitongoji cha Dahieh,kwenye wakazi wengi wa madhehebu ya Kishia.Tangu mapigano kuanza majuma matatu yaliyopita,eneo hilo limeshambuliwa na Israel mara kwa mara.Kwa upande mwingine,siku ya Jumatano,wanamgambo wa Hezbollah walirusha kama makombora 230 kaskazini mwa Israel.Hiyo ni idadi kubwa kabisa ya makombora kupata kuvurumishwa na Hezbollah katika siku moja.