1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

BEIRUT: Mwanawe Hariri aisifu ripoti ya umoja wa mataifa juu ya uchunguzi wa kifo cha babake

22 Oktoba 2005

Mwanawe aliyekuwa waziri mkuu nchini Lebanon, marehemu Rafiki Hariri, ameisifu ripoti ya umoja wa mataifa inayoituhumu Syria kwa kuhusika katika mauaji ya babake.

Saad al-Hariri ameitaka mahakama ya kimataifa iwaadhibu wauaji wa babake akisema yeye pamoja na jamii yake wanataka haki ifanyike na wala hawataki kulipiza kisasi. Ripoti hiyo iliyowasilishwa na mchunguzi wa Ujerumani, Detlev Mehles, imetaja ushahidi kwamba serikali ya Syria na Lebanon zilihusika katika kifo cha Hariri.

Balozi wa Syria nchini Marekani, Imad Moustapha, ameieleza ripoti hiyo kuwa na msukumo wa kisiasa. Gazeti linalomilikiwa na serikali nchini Misri, Al-Ahram, limesema ripoti hiyo haikutayarishwa kufuatia ushawishi wowote wa kisiasa na linataka waliohusika waadhibiwe.

Baraza la mawaziri nchini Lebanon linakutana kwa dharura kuijadili ripoti hiyo, huku rais Emile Lahud akikabiliwa na shinikizo la kujiuzulu. Mkutano huo maalumu unafanyika wakati baraza la usalama la umoja wa mataifa likijiandaa kuijadili ripoti hiyo Jumanne ijayo ili kuamua hatua itakazochukua kuhusiana na ripoti hiyo.

Syria bado inashikilia kwamba haikuhusika kwa njia yoyote katika kifo cha Hariri na ikasema itaendnelea kushirikiana na jamii ya kimataifa.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW