BEIRUT: Nasrallah aionya Israel
10 Agosti 2006Kiongozi wa kundi la Hezbollah, Sayyed Hassan Nasrallah, ameapa kuligeuza eneo la kusini mwa Lebanon kuwa makaburi ya wanajeshi wa Israel na kuvurumisha maroketi zaidi mjini Haifa.
Amewaonya wanajeshi wa Israel kwamba hawataweza kukaa nchini Lebanon na watakapoingia wanambambo wa Hezbollah watawaondoa kwa nguvu.
Nasrallah amesema wanataka kumaliza mashambulio lakini kama kuna lazima ya kupigana basi wako tayari kujibwaga uwanjani. Amewaonya warabu wanaoishi mjini Haifa waondoke ili wasiumizwe na maroketi ya Hezbollah.
Wakati huo huo, kundi la Hezbollah limekanusha madai ya Israel kwamba wapiganaji wa Iran ni miongoni mwa wanamgambo wa Hezbollah wanaopigana na wanajeshi wa Israel kusini mwa Lebanon.
Runinga ya Israel ilizinukulu duru za kidiplomasia zikisema kwamba wapiganaji wa Iran waligunduliwa nchini Lebanon miongoni mwa maiti wakati stakabadhi zilipopata milini mwao.
Hata hivyo hakuna habari zaidi zilizotolewa juu ya idadi yao na wakati walipotambuliwa. Jeshi la Israel halijatoa taarifa yoyote juu ya matamshi hayo ya Hezbollah.
Wakati haya yakiarifiwa, Canada imetangaza kwamba itawahamisha raia wake 2,400 kutoka Beirut wiki ijayo kutumia boti.