Beirut: Wanamgambo wa Fatah al-Islam washambulia kituo cha nguvu za umeme, Lebanon.
2 Agosti 2007Wanamgambo wanaoungwa mkono na kundi la Al Qaeda wanaokabiliana na majeshi ya Lebanon wameshambulia kituo cha nguvu za umeme kaskazini mwa nchi hiyo na kusababisha kukatizika huduma ya umeme.
Vikosi vya usalama vimesema wanamgambo wa Fatah al-Islam walio katika kambi ya wakimbizi ya Nahr al-Bared walivurumisha makombora kadhaa kuelekea kituo hicho cha nguvu za umeme.
Wakati huo huo, afisa wa kijeshi wa Lebanon ameuawa kwenye makabiliano katika kambi hiyo.
Watu kiasi mia mbili na hamsini na watatu, wakiwemo wanajeshi mia moja na ishirini na wawili, wameuawa tangu vita hivyo vilipoanza mwezi Mei.
Huo ndio mzozo mbaya zaidi kuwahi kuikumba nchi hiyo tangu mwaka 1990 wakati vita vya wenyewe kwa wenyewe vya muda wa miaka kumi na mitano vilipomalizika.