Beirut:Kudharauliwa kwa kauli ya Annan na Israel.
18 Julai 2006Mashambulizi ya ndege za kijeshi za Israel nchini Lebanon zimeuwa watu wengine 11, wakati nchi kadhaa ulimwenguni zikijaribu kuondosha raia wake nchini humo.
Katika siku sita zilizopita jumla ya raia wa Lebanon 210 wamefariki dunia wakati ni raia 24 tu wa Israel ndio waliofariki katika majibizano ya mashambulizi.
Mashambulizi ya mwisho ya Israel nchini Lebanon yalilenga huko Aitaroun, pia kijiji cha mpakani mwa Lebanon na makaazi ya walebanon karibu na Beirut.
Wanamgambo wa Hezbollah wameendelea kurusha roketi zaidi huko kusini mwa Lebanon, na kupiga kaskazini mwa Israel ukiwemo mji wa Haifa.
Watu wanne wamejeruhiwa, na roketi nyengine ilipiga karibu na hospitali ya Safed na kujeruhi watu watano.
Wakati mashambulizi yakiendelea, meli iliyobeba raia wa Ufaransa na Italy imeondoka kutoka Beirut kuelekea Syprus.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Kofi Annan ametaka kupelekwa kwa kikosi kipya cha kulinda amani huko kusini mwa Lebanon, lakini waziri mkuu wa Israel Ehud Olmert amepinga tena tamko hilo hadi pale wanajeshi wake wawili watakapoachiliwa huru.
Nacho kikundi cha wanamgambo wa Hezbollah wamekataa mapatano yoyote na Israel.
Kuhusu juhudi za kibalozi zinazofanywa kusimamisha mapigano katika Lebanon, Muwakilishi wa Umoja wa Ulaya kuhusu usalama na masuala ya kigeni Havier Solana alisema:
“Sisi tutafanya kila kitu kinachowezekana licha ya kwamba misimamo ya Israel na Chama cha Hezbollah kuhusu kusimamisha mapigano, yako mbali kabisa. Hata hivyo ni muhimu kwamba serikali ya Lebanon itoe mchango mkubwa.”
Wakati huo huo umoja wa nchi za ulaya umeidhinisha Euro milioni tano kwa kuwapatia huduma wahanga wa Lebanon walioathirika kutokana na mashambulizi ya ndege za kijeshi za Israel, yaliyopelekea kubomolewa kwa miundo mbinu kama barabara, madaraja, umeme na njia za kusambazia maji.