BEIRUT:Watu 40 waeuawa katika mapigano huko Lebanon
21 Mei 2007Mapigano makali yameendelea hii leo kwenye kambi ya wakimbizi wa kipalestina katika mji wa Tripoli huko kaskazini mwa Lebanon ambapo watu 40 wameuawa.
Mapigano hayo ni kati ya wanajeshi wa Lebanon na wanamgambo wa Kipalestina, baada ya askari wa Lebanon kufanya msako dhidi ya makundi ya waporaji mabenki.
Miongoni mwa waporaji hao ni wakimbizi wa kipalestina waliojitenga na kundi la Fatah na kuanzisha kundi la Fatah al Islam.
Kundi hilo ambalo linashutumiwa kuwa na uhusiano na kundi la Al Qaida lililaumu msako huo likisema ni uchokozi.
Wengi waliyouawa katika mapigano hayo ni askari wa pande hizo mbili, ambapo madaktari katika kambi hiyo ya Nahr al Bared wamesema kuwa raia sita wameuawa.
Bunge la Lebanon limesema kuwa kundi hilo linajaribu kuweka hali tete ya kisiasa nchini humo, mnamo wakati ambapo kuna uhasama wa kisiasa kati ya serikali ya Lebanon inayoungwa mkono na nchi za magharibi na wapinzani wanaoungwa mkono na Syria.
Serikali ya Lebanon iko katika mbinyo wa Umoja wa Mataifa kuwafikisha mbele ya sheria wauaji wa waziri mkuu wa zamani wa nchi hiyo, Rafik Harir mwaka 2005.
Wakati huo huo mwanamke mmoja ameuawa na watu wengi 10 kujeruhiwa baada ya kutokea mlipuko katika eneo la maduka mashariki mwa mji mkuu Beirut.Eneo hilo linakaliwa na idadi kubwa ya wakristo.