1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Belarus: Lukashenko asema haondoki ng'o madarakani

Zainab Aziz Mhariri: Josephat Charo
8 Septemba 2020

Rais wa Belarusi Alexander Lukashenko anayekabiliwa na upinzani amesema haondoki madarakani ng‘o licha ya kuwepo wimbi la maandamano linalopinga utawala wake, 

Belarus Präsident Lukaschenko
Picha: Reuters/BelTA/N. Petrov

Rais huyo wa Belarus Alexandar Lukashenko wakati wa mahojiano na waandishi wa habari wa Urusi, amesema wafuasi wake watashambuliwa ikiwa ataondoka. Lukashenko ameitawala Belarus tangu mwaka 1994 na alidai kushinda katika uchaguzi wa Agosti 9 ambao wapinzani wake wanasema madai ya kiongozi huyo si ya kweli na kwamba upande wa upinzani uliibiwa kura na hivyo kuporwa ushindi huo.

Kiongozi wa upinzani wa Belarus aliyeko uhamishoni Svetlana Tikhanovskaya amesema kumekuwa na maandamano nchini Belarus kila siku tangu uchaguzi wa urais ulio na utata uliofanyika mwezi uliopita. Waandamanaji wapatao 7,000 wamewekwa kizuizini. Wakati huo huo Umoja wa Mataifa umepokea takriban ripoti 450 za watu kuteswa na unyanyasaji wa aina nyingine kwa watu hao waliozuiliwa.

Rais wa Baraza la Bunge la Ulaya, Rik Daems, amesema kuwa watu wa Belarus wamefikia hatua ambapo hawaogopi tena kutetea haki yao. Amesema kwa mtazamo wake juhudi za aina hii sio za kuvuruga amani bali ni juhudi za kusisitiza wito wa kuleta mabadiliko.

Kiongozi wa upinzani nchini Belarus Maria KolesnikovaPicha: AFP/Tut.by

Mwakilishi wa serikali ya Belarus, Andrei Savinykh, mwanachama wa ngazi ya juu wa bunge la kitaifa la nchi hiyo, amesema polisi wa Belarus walizingatia misingi ya haki katika juhudi za kutuliza vurugu zilizoanzishwa na waandamanaji. Savinykh amesema, waandamanaji wanatiwa moyo na watu kutoka nje, haswa kutoka nchi jirani ya Poland ambayo ni mwanachama wa Umoja wa Ulaya na amelituhumu jeshi la Poland kwa kuhusika lakini Poland imekanusha madai hayo.

Maria Kolesnikova, mwanachama wa Baraza la Uratibu lililoundwa na upinzani kwa ajili ya kuwezesha mazungumzo na kiongozi wa muda mrefu wa Belarus Alexander Lukashenko juu ya mabadiliko kwenye uongozi wa nchi hiyo, alikamatwa hapo jana Jumatatu katika mji mkuu, Minsk, pamoja na wajumbe wengine wawili wa baraza hilo.

Umoja wa Ulaya unataka kuachiwa mara moja kwa watu waliokamatwa. Mkuu wa sera za nje wa Umoja wa Ulaya Josep Borrel ameitaka serikali ya Belarus iwaachie wapinzani wote waliotiwa ndani. Amesema jumuiya hiyo ya Umoja wa Ulaya inaweza kuiwekea Belarus vikwazo. Borrel ameeleza kuwa vikwazo hivyo vinaweza kuwekwa wiki ijayo.

Vyanzo:RTRE/DPA/AP

 

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW