1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Belarus yaanza kuwarudisha wahamiaji walikotoka-Ripoti

Daniel Gakuba
23 Novemba 2021

Wizara ya mambo ya ndani ya Belarus imesema kuwa wahamiaji 118 wameondoka nchini humo na kurudi walikotoka. Nchi hiyo imekuwa na mzozo na Umoja wa Ulaya, unaoituhumu kusababisha mzozo wa wahamiaji kwa makusudi.

Belarus Migranten in der Nähe der weißrussisch-polnischen Grenze in der Region Grodno
Picha: Kacper Pempel/REUTERS

Taarifa ya kuondoka kwa wahamiaji hao imetolewa na shirika la habari la Urusi, TASS ambalo limesema kuwa kundi la kwanza la wahamiaji hao liliondoka Jumatatu, na kundi jingine linatarajiwa kufuata leo Jumanne.

Nchi za Umoja wa Ulaya zinazopakana na Belarus, zikiwemo Poland, Lithuania na Latvia zimeishutumu Belarus kusababisha mzozo wa wahamiaji kwenye mpaka wao, kama hila ya kuushinikiza Umoja wa Ulaya kuiondolea vikwazo serikali ya Rais Alexander Lukashenko, ilivyowekewa baada ya uchaguzi wenye utata wa mwaka 2020 uliompa ushindi kiongozi huyo wa kiimla ambaye amekuwa madarakani tangu mwaka 1994. Uchaguzi huo ulifuatiwa na ukandamizaji mkubwa dhidi ya waandamanaji wa upinzani waliokataa ushindi wa Lukashenko.

Mzozo wa wahamiaji umeifanya Poland kujenga uzio mpakani na kuweka maelfu ya walinziPicha: Leonid Shcheglov/AP/picture-alliance

Umoja wa Ulaya wakataa shinikizo la Belarus

Umoja wa Ulaya umekataa kuzungumza na Belarus kuhusu mzozo huo wa wakimbizi waliopiga kambi kwenye mpaka, lakini msemaji wa umoja huo amesema kuwa wamekuwa na mawasiliano na baadhi ya wadau kutoka upande wa Belarus, na kuwa upo uwezekano wa kuzungumza na mashirika ya Umoja wa Mataifa na maafisa wa Belarus kwenye ngazi ya kiufundi, juu ya namna ya kusaidia kuwarejeshawahamiaji hao walikotoka.

Soma zaidi: Utulivu warejea kwenye mpaka wa Poland na Belarus

Rais Lukashenko amekasirishwa na uamuzi huo wa Umoja wa Ulaya wa kukataa kuwapokea wakimbizi hao, akidai aliahidiwa na Kansela wa Ujerumani Angela Merkel katika mazungumzo yao kwa njia ya simu, kuwa nchi za Ulaya zingelitafakari suala hilo. Msemaji wa Kansela Merkel Steffen Seibert amekanusha madai hayo ya Lukashenko.

Kansela Angela Merkel wa Ujerumani amekosolewa kwa kuzungumza na Lukashenko kuhusu hali ya wahamiaji mpakani

''Hili wazo la kuwepo njia ya kibinadamu ya kuwapeleka wahamiaji 2000 nchini Ujerumani, sio suluhisho linalokubalika, iwe kwa Ujerumani au kwa Umoja wa Ulaya. Hayo pia yalielezwa bayana wakati waziri wa mambo ya ndani wa Ujerumani Horst Seehofer alipomtembelea mwenzake wa Poland wiki iliyopita,'' amesema Seibert.

Merkel apondwa kwa kuzungumza na Lukashenko

Hatua ya Kansela Merkel ya wiki iliyopita kuzungumza na Rais Lukashenko, ambaye Umoja wa Ulaya hauutambui ushindi wake katika uchaguzi wa mwaka jana, imekosolewa sana na kiongozi wa upinzani wa Belarus Svetlana Tikhanovskaya anayeishi uhamishoni tangu mwaka jana. Bi Tikhanovskaya amesema kwa mtazamo wa wanaharakati wa Belarus, ingefaa viongozi wa Ulaya wajiepushe kuwasiliana na Lukashenko.

Soma zaidi: Lukashenko kufanya mazungumzo na Merkel juu ya uhamiaji

Jana Jumatatu, Kansela Merkel alifanya mazungumzo kwa njia ya simu na mwanaharakati huyo, kumhakikishia kuwa bado Ujerumani inaunga mkono kwa dhati juhudi za kuleta demokrasia nchini Belarus, hayo yakiwa ni kwa mujibu wa msemaji wa Kansela Merkel, Steffen Seibert.

 

afpe, dpae, rtre

 

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW