1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Belarus yamfunga jela Tsikhanouski, mpinzani wa Lukashenko

14 Desemba 2021

Mahakama moja nchini Belarus imemhukumu kiongozi wa upinzani Siarhei Tsikhanouski kifungo cha miaka 18 jela.

Belarus-politics-CZECH-BELARUS-POLITICS-DIPLOMACY
Picha: Roman Vondrous/POOL/AFP via Getty Images

Tsikhanouski- alikamatwa mwaka uliopita baada ya kuongoza vuguvugu ambalo halikutarajiwa dhidi ya Alexander Lukashenko.

Shirika la habari linalomilikiwa na serikali Belta limeripoti kwamba mnamo siku ya Jumanne mahakama ilimhukumu Siarhei Tsikhanouski ambaye ni mkosoaji wa serikali ya Belarus, kifungo cha miaka 18 jela. Hayo yamejiri baada ya kukamilika kwa kesi dhidi yake iliyoendeshwa faraghani.

Ulaya yaongeza vikwazo Belarus

Mke wa Tsikhanouski Sviatlana Tsikhanouskaya- ambaye alikuwa mchanga kisiasa wakati wa kukamatwa kwa bawanake, alichukua nafasi yake kama mgombea kuwania urais akijinadi kuwa mgombea bora katika uchaguzi huo.

Amepinga uamuzi huo wa mahakama. "Dikteta hulipiza kisasi hadharani dhidi ya wapinzani wake wakuu," ameandika kwenye ukurasa wake wa twitter punde tu baada ya uamuzi huo kutolewa mahakamani.

"Huku akiwaficha wafungwa wa kisiasa na kesi dhidi yao kuendeshwa faraghani, anatumai kuendeleza ukandamizaji wa kimyakimya. Lakini ulimwengu mzima unatizama. Hatutakoma," ameongeza hivyo kwa lugha ya Kiingereza.

Mwanaharakati wa Belarus apatikana amekufa Ukraine

Serikali ya Lukashenko inashutumiwa kwa kukandamiza uhuru huku wakosoaji wa Lukashenko wakifungwa jela au kulazimishwa kuikimbia nchi.Picha: Pavel Bednyakov/dpa/Sputnik/picture alliance

Je Siarhei Tsikhanouski alikutikana na hatia gani?

Tsikhanouski mwenye umri wa miaka 43 amekuwa kizuizini tangu Mei mwaka 2020 baada ya kukutikana na hatia ya kuongoza maandamano makubwa na uchochezi.

Tsikhanouski alipanga kuwania urais dhidi ya Lukashenko Agosti mwaka 2020 nchini Belarus. Lakini alikamatwa kabla ya uchaguzi kufanyika na kufungwa.

Wakati wa kampeni zake, Tsikhanouski alibuni tusi jipya dhidi ya Lukashenko kwa kumuita ‘kombamwiko’. Kauli mbiu yake ikawa ni mkomeshe kombamwiko huku wafuasi wake wakijibu kwa kubeba ndara za miguuni, ambazo wakati mwingine hutumika kuwaua wadudu.

Punde tu alipotangaza kuwa atawania urais, mwanaharakati huyo aliwekwa kizuizini na kushtakiwa kwa makosa ya kuvuruga utulivu wa umma.

Washirika wa Tsikhanouski pia wapewa hukumu

Maandamano makubwa yalifanyika Minsk na miji mingine kupinga utawala wa Lukashenko.Picha: TASS/dpa/picture alliance

Wapinzani kadhaa wa Lukashenko pia walihukumiwa kortini. Mikola Statkevich ambaye ni mmoja kati ya wapambe watano wa Tsikhanouski ambaye alikabiliwa na kesi, alihukumiwa kifungo cha miaka 14 jela.

Statkevich mwenye umri wa miaka 65 alikuwa mpinzani wa Lukashenko katika uchaguzi wa mwaka 2011, lakini alifungwa miaka 6 gerezani. Alipoachiliwa huru mwaka 2015 alipigfwa marufuku kuwania urais katika uchaguzi wa 2020.

Viongozi walaani kukamatwa mwanaharakati wa Belarus

Mwanaharakati mwengine aliyefunguliwa mashtaka ni Ihar Losik mwenye umri wa miaka 29 ambaye amehukumiwa kifungo cha miaka 15 jela. Aliwekwa kizuizini  katikati ya mwaka 2020 kwa tuhuma za kutumia app ya simu ya Telegram kwa kuchochea maandamano.

Wengine ni mwandishi wa blogu Uladzimir Tsyhanovich aliyehukumiwa kifungo cha miaka 15 jela, wanaharakati Artsiom Sakau na Dzmitry Papou ambao ni washirika wa Tsikhanouski. Wao pia wamehukumiwa kifungo cha miaka 16 jela kila mmoja.

Mkewe Tsikhanouski aahidi kuendelea na mapambano

Mkewe Tsikhanouski aahidi kuendelea kupambana kuikomboa BelarusPicha: Julien Warnand/REUTERS

Kabla ya uamuzi huo Sviatlana Tsikhanouskaya alisema kwamba hukumu itakayotolewa itakuwa kinyume cha sheria na haiwezi kuleta amani.

"Nitaendelea kumpigania mpenzi wangu ambaye alikuwa kiongozi wa mamilioni ya watu wa Belarus,” Tsikhanaouskaya alisema kwenye vídeo.

"Nitajaribu kufanya kitu kigumu, labla kisichowezekana kuleta mabadiliko ambapo tutaweza kuleta Belarus mpya,”amesema.

Raia wa Belarus wamshtaki Lukashenko Ujerumani

Tsikhanouskaya, ambaye alikuwa mama wa nyumbani akiwalea Watoto wake wawili wakati bwana yake alipotiwa nguvuni, alilazimika kukimbia Belarus baada ya jaribio la kuwania urais akenda Lithuania.

Mashaka kuhusu matokeo ya uchaguzi yalisababisha maandamano makubwa Belarus yakiwavutia hadi watu 200,000 mjini Minsk.

Utawala wa Lukashenko uliyajibu maandamano hayo kwa kutumia nguvu dhidi ya waandamanaji na Zaidi ya 30,000 walikamatwa huku maelfu wakipigwa vibaya.

Umoja wa Ulaya wahofia ukandamizaji, Belarus

Serikali ya Lukashenko imewafunga jela au kuwalazimisha wapinzani wake wakuu kuikimbia nchi. Nazo mahakama za Belarus zimekosolewa mara kwa mara kwa kuingiza siasa kwenye maamuzi yao.

Katika kesi moja, Maria Kolesnikova alihukumiwa kifungo cha miaka 11 ngerezani mwezi Septemba kwa hatia ya kuenda kinyume na sheria ya usalama wa taifa na pia kupanga njama ya kunyakua mamlaka.

Mnamo Julai, kiongozi mwengine wa upinzani ambaye ni muhudumu wa zamani wa benki Viktor Babariko alifungwa miaka 14 jela kufuatia madai ya ufisadi.

rc/msh (dpa, AFP)

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW