1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Belarus yavutana na mshirika wake wa jadi Urusi

Sylvia Mwehozi
30 Julai 2020

Belarus imesema hii leo kuwa inashuku kundi la wapiganaji mamluki wa Urusi iliowakamata siku moja iliyopita, lilikuwa likipanga njama za ugaidi dhidi ya nchi hiyo, kuelekea uchaguzi wa rais wa mwezi Agosti.

Russland - Alexander Lukaschenko und Vladimir Putin
Picha: picture-alliance/dpa/S. Karpukhin

Belarus ilisema Jumatano kuwa imewakamata zaidi ya wapiganaji 30 wanaoshukiwa kuwa mamluki wa Urusi, karibu na mji mkuu wa nchi hiyo Minsk baada ya kupokea taarifa kuwa wapiganaji zaidi ya 200 wameingia nchini humo kwa ajili ya kuvuruga uchaguzi wa rais uliopangwa Agosti 9.

Mvutano huo mpya unatishia kudhoofisha mahusiano na mshirika wake wa jadi Urusi, ambayo hadi sasa haijatoa msimamo wake. Tayari Belarus imemuita balozi wa Urusi nchini humo kwa ajili ya kutoa maelezo. 

Mkuu wa baraza la kitaifa la usalama la Belarus Andrei Ravkov amewaeleza waandishi wa habari kuwa, karibu wapiganaji mamluki 200 bado wako nchini humo na kwamba maafisa wa usalama wanaendelea na msako. Vyombo vya habari vya ndani navyo vimeeleza kuwa wapiganaji waliokamatwa ni wafanyakazi wa kampuni binafsi ya kijeshi ya Urusi ya Wagner.

Rais Alexander Lukashenko ambaye ameitawala Belarus tangu mwaka 1994, anatafuta muhula mwingine madarakani katika uchaguzi wa Agosti 9 lakini anakabiliwa na upinzani mkali wakati huu, mnamo pia umma ukiwa umekasirishwa na namna alivyokabiliana na janga la COVID-19, uchumi na masuala ya haki za binadamu.

Rais wa Belarus Alexander Lukashenko akiwa na baraza la usalamaPicha: Reuters/N. Petrov

Vikosi vya usalama vilitawanya kile walichokiita maandamano haramu katika wiki za hivi karibuni. Lukashenko anawatuhumu waandamanaji kwa kula njama za kutaka kumpindua. Mwezi uliopita aliituhumu Urusi na vikosi vya Poland kwa kujaribu kumdhoofisha. Urusi inakana madai hayo.

Kufuatia mvutano huo wa sasa na Urusi, Belarus imetangaza kuimarisha usalama katika mpaka wake na Urusi na rais Lukashenko ameamuru udhibiti mkali wa matukio yote ya umma, na kusisitiza kuwa mamlaka husika zitoe maelezo.

"Ninaangalia majibu ya warusi, tayari wameanza kujitetea kwamba tuliwaleta hapa. Kama ni raia wa urusi na naelewa kuwa tayari wamehojiwa, basi ni muhimu kuwasiliana mara moja na vyombo husika vya Urusi ili kujua nini kinaendea," alisema Lukashenko.

Belarus na Urusi ni washirika wa jadi, lakini mahusiano yao yaliingia doa kitambo kutokana na sababu kadha ikiwemo uamuzi wa Lukashenko wa kukataa kuunga mkono hatua ya Urusi ya kuitwaa rasi ya Crimea ya nchini Ukraine mwaka 2014 na wito wa Urusi wa kutaka ushirikiano wa kisiasa na kiuchumi na Belarus.

Wanajeshi binafsi wa Urusi wamekuwa wakipigana katika mizozo tofauti kama vile Syria, Ukraine na Libya, kulingana na taarifa ya vyombo vya habari vya kigeni.

 

 

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW