1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kiongozi wa upinzani Belarus akamatwa mpakani na Ukraine

Zainab Aziz Mhariri: Josephat Charo
8 Septemba 2020

Vyombo vya habari vya serikali nchini Belarus vimeripoti kwamba Maria Kolesnikova amekwamtwa siku moja baada ya kushuhudiwa akipakiwa kwa nguvu kwenye basi dogo na watu waliokuwa wamefunika nyuso zao

Belaurs Minsk | Proteste - Maria Kolesnikowa
Picha: Getty Images/AFP/S. Gapon

Kwa mujibu wa taarifa zaidi kiongozi huyo wa upinzani alikamatwa na walinzi wa mpakani wakati alipokuwa anajaribu kuondoka nchini kinyume cha sheria. Wapinzani bado hawajathibitisha habari hizo.

Wapambe wawili wa bibi Kolesnikova pia walitiwa nguvuni ambao ni katibu wa habari na katibu mtendaji. Hata hivyo wapambe hao sasa wako nchini Ukraine.

Kolesnikova alitoweka jana Jumatatu katika mji wa Minsk baada ya kuonekana akiwa anaingizwa kwa lazima kwenye basi dogo. Kiongozi mkuu wa upinzani wa Belarus aliye uhamishoni Svetlana Tikhanovskaya ametoa wito wa kuwekwa vikwazo na shinikizo la kimataifa dhidi ya Rais Alexander Lukashenko na maafisa wanaohusika katika na vitendo vya ukandamizaji dhidi ya upinzani.

Rais wa Belarus Alexander LukashenkoPicha: picture-alliance/AP Images/N. Petrov

Kiongozi wa upinzani wa Belarus aliye uhamishoni amesema viongozi wa upinzani wanashikiliwa kwa mashtaka ya uwongo, wanatishwa, na hata kufukuzwa kutoka nchi kwenye nchi yao. Kiongozi huyo wa upinzani Tikhanovskaya amehimiza juu ya kuachiwa huru mara moja kwa wafungwa wote wa kisiasa nchini Belarus. Amesema watu wa Belarus sasa wanahitaji msaada, na amesisitiza juu ya kuwajibishwa watu ambao hutoa amri za jinai ambazo zinakiuka kanuni za kimataifa na haki za binadamu.

Kiongozi maarufu wa upinzaji wa Belarus Maria Kolesnikova imeripotiwa ameichanachana pasipoti yake ili kuzuia jaribio la kumpeleka kwa nguvu katika nchi jirani ya Ukraine, hayo ni kwa mujibu wa shirika la habari la Interfax la nchini Ukraine.

Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani wa Ukraine Anton Gerashchenko ameandika kwenye mtandao wa Facebook kwamba Kolesnikova, aliyekuwa amepotea katika saa 24 zilizopita, amefanikiwa kuzuia kufukuzwa kwa nguvu kutoka katika nchi yake ya asili.

Kiongozi wa upinzani wa Belarus aliye uhamishoni Svetlana Tikhanovskaya amesema Lukashenko hana uhalali wowote wa kuwa rais wa Belarus.

Vyanzo:AP/DPA/RTRE/AFP