Bemba ahukumiwa miaka 18 jela
21 Juni 2016Bemba ni afisa wa ngazi ya juu kuhukumiwa katika mahakama hiyo ya ICC baada ya kupatikana na hatia mwezi Machi kwa mashitaka matano ya uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya ubinadamu. Hii ni adhabu kubwa na ya kwanza ya mahakama hiyo kutolewa dhidi ya kiongozi wa juu.
Hatia ya makosa
Alihukumiwa hapo Machi kwa makosa matano ya uhalifu wa vita na uhalifu wa kibinadamu, baada ya kutuma kikosi cha askari 1500 kutoka katika jeshi lake binafsi kwenda Afrika ya kati katika kile kinachodaiwa kusaidia kufanya mapinduzi dhidi ya rais wa wakati huo wa nchi hiyo.
Askari wa jeshi lake binafsi wanadaiwa kutekeleza ubakaji na mauaji na kudaiwa kushiriki mapinduzi ya rais Ange-Felix Patasse.
Wataalamu walithibitisha kwamba matukio hayo ya ukatili yangeleta athari za muda mrefu kwa jamii na waathirika wenyewe.
Katika hukumu iliyotolewa mwishoni mwa kesi hiyo iliyoanza mwezi Novemba mwaka 2010, majaji wa mahakama ya ICC waliona kwamba licha ya kufahamu kile kilichokuwa kikiendelea, Bemba alishindwa kuchukua hatua zozote za kuzuia aina yoyote ya uhalifu, ikiwemo magenge ya ubakaji wa wanaume, wanawake na watoto, wakati mwingine ndugu zao wakilazimishwa kuangalia.
Wanaharakati walisema hukumu ya miaka 25 iliyopendekezwa awali na waendesha mashitaka haikulingana na uzito wa makosa yanayomkabili.
Mahakama hiyo iliwahi kutoa hukumu ya miaka 14 na 12 gerezani kwa washitakiwa wengine wawili.
Pamoja na kulichukulia suala la ubakaji kama silaha ya kivita, Kesi ya kiongozi huyo pia imekuwa ya kwanza katika mahakama ya ICC kumlenga moja kwa moja kamanda wa kijeshi kwa makosa yaliyofanywa na askari wake, hata kama hakutoa amri yoyote.
Mawakili upande wa utetezi wanadai kwamba Bemba ambaye amekuwa kizuizini kwa miaka nane tangu kukamatwa kwake mwaka 2008 mjini Brussels, alipaswa kuachiwa.
Mmoja wa mawakili Peter Haynes aliiambia mahakama hiyo mwezi uliopita kuwa "Bemba hakushiriki katika makosa hayo. Hakuwepo kutoa amri wala kuwahamasisha askari wake" alisema kwamba hata hakuwepo katika nchi yalikofanyika makosa hayo.
Wanaharakati hata hivyo walionya kwamba hukumu nyepesi itashindwa kutoa onyo kwa makamanda wengine wa kijeshi
"Ni muhimu kwa mahakama kutambua wajibu wa kamanda, na kuna nafasi ya kuzuia" alisema Carrie Comer mwakilishi wa kudumu wa ICC kwa Shirikisho la Kimataifa la Haki za Binadamu (FIDH).
"Kama alijua au angefahamu, mambo haya yalitokea na yeye ndio mdhibiti mkuu kwa kikosi cha jeshi, ndio, anawajibika kabisa kwa kutozuia au kuwaadhibu waliotenda makosa hayo" anasema mwanaharakati huyo.
Kesi hiyo ya Bemba iliwashangaza wengi kwa kuchukua muda mrefu kutambua uhalifu wa ngono katika mahakama ya kimataifa.
Mwandishi:Sylvia Mwehozi/AFP
Mhariri:Saumu Yusuf