1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ben Ali akimbilia Saudi Arabia

15 Januari 2011

Saudi Arabia imetangaza rasmi kuwa imemkaribisha Rais wa Tunisia aliyepinduliwa, Zine El Abidine Ben Ali na familia yake, baada ya kushinikizwa kuondoka madarakani.

Zine El Abidine Ben Ali, aliyekuwa rais wa TunisiaPicha: picture alliance / dpa

Taarifa ya jumba la kifalme iliyotangazwa na shirika la habari la nchi hiyo SPA imethibitisha kuwa Ben Ali aliwasili nchini humo mapema leo, baada ya kuondoka Tunisia hiyo jana na hivyo kumalizika kwa utawala wake wa miaka 23, kufuatia maandamano makubwa yaliyosababisha umwagaji damu.

Taarifa hiyo ilieleza kuwa kutokana na wasiwasi wa mazingira ya kipekee yanayowakabili ndugu zao wa Tunisia na katika kuunga mkono usalama na utulivu nchini mwao, serikali ya Saudi Arabia imempokea Rais Ben Ali na familia yake. Rais Ben Ali anaondoka madarakani baada ya kuongoza kwa zaidi ya miongo miwili. Kabla ya kuondoka nchini humo alimkabidhi madaraka ya muda Waziri Mkuu wa Tunisia Mohammed Ghannouchi.

Waziri Mkuu wa Tunisia, Mohamed Ghannouchi kuiongoza serikali ya mpitoPicha: AP

Akizungumza na wananchi wa Tunisia Ghannouchi alisema ataiongoza kwa muda nchi hiyo hadi hapo uchaguzi wa mapema utakapofanyika na kwamba anachukua madaraka kutokana na rais kutoweza kutekeleza majukumu yake. Aidha, amewatolea wito wananchi wa Tunisia kutoka vyama vyote vya kisiasa kuungana pamoja ili kuiruhusu nchi hiyo kukishinda kipindi hiki kigumu na kurejea katika utulivu. Mitaa ya mji mkuu wa Tunis ilikuwa shwari, huku kukiwa na usalama wa hali ya juu, lakini wachambuzi wanahoji iwapo mabadiliko hayo ya uongozi wa juu, yatawaridhisha waandamanaji.

Serikali ya Ben Ali ambaye amekuwa madarakani tangu mwaka 1987, ilitangaza hali ya hatari hapo jana na ilitoa amri ya kutotoka nje kuanzia usiku hadi alfajiri. Hatua hiyo ilichukuliwa baada ya siku kadhaa za vurugu zilizoanzia miji mingine na kusambaa hadi Tunis na kusababisha watu kuuawa wakati vikosi vya usalama vilipojaribu kuwadhibiti waandamanaji hao wenye hasira.

Kipindi cha mabadiliko ya utawala

Kiongozi wa chama cha upinzani nchini Tunisia cha Democratic Progressive, Mohammed Nejib Chebbi, amekielezea kitendo hicho kama mabadiliko ya serikali. Akizungumza na kituo kimoja cha televisheni cha Ufaransa, Bwana Chebbi amesema hiki ni kipindi muhimu kwani kuna mabadiliko ya utawala.

Rais Barack Obama wa MarekaniPicha: AP

Wakati huo huo, Rais Barack Obama wa Marekani ametoa wito wa kufanyika uchaguzi ulio huru na wa haki nchini Tunisia. Rais Obama pia amepongeza ujasiri na utu wa Watunisia. Alisema analaani matumizi ya nguvu dhidi ya raia ambao wanaelezea maoni yao kwa njia ya amani nchini humo. Aidha, amevisihi vyama vyote kubakia shwari na kuepuka ghasia na ameitaka serikali ya Tunisia kuheshimu haki za binaadamu na kuandaa uchaguzi huru na wa haki hivi karibuni.

Kwa upande wake, Umoja wa Ulaya umetaka kupatikana kwa ufumbuzi wa amani nchini Tunisia wakati ambapo kiongozi wake ameondoka nchini humo. Mkuu wa sera za kigeni wa umoja huo, Catherine Ashton amevitaka vyama vyote kuonyesha uvumilivu na kubakia shwari ili kuepusha ghasia na vifo zaidi. Bibi Ashton amesema mazungumzo ni muhimu na Umoja wa Ulaya upo tayari kuisaidia Tunisia na umma wake kupata suluhisho la kudumu la demokrasia katika mzozo unaoendelea.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo (AFPE,RTRE)
Mhariri: Prema Martin